OFISA Usalama, Saidi Saidi (36) amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na mafuta ya simba yenye thamani ya Sh milioni 10.7.
Hukumu hiyo ilitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri. Hakimu Mashauri alisema upande wa mashitaka umeweza kukidhi mashitaka bila ya kuacha shaka baada kusikiza mashahidi wa upande wa mashitaka na utetezi.
“Nakuhukumu kifungo cha miaka 20 jela ili iwe fundisho kwako na wengine wanaofanya matukio kama haya na kuonesha kwamba tuko makini kupinga vitendo hivi,” alisema Hakimu Mashauri.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali, Adolf Mkini aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa jamii inayojihusisha na matukio kama hayo.
Hata hivyo, mshitakiwa Saidi alidai ana familia inayomtegemea ya wazazi na watoto wake na kwamba anaomba apunguziwe adhabu. Inadaiwa kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu 86 (1) (2) (c) (ii) ya Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya 2009.
Inadaiwa February 8, mwaka jana katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, Said alikamatwa akiwa na mafuta ya Simba yenye thamani ya Sh milioni 10.7 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.