RAIS John Magufuli ameagiza kuanzia kesho taasisi zote zinazotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam ziungane na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) kutoa huduma kwa saa 24 ili kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji wa mizigo bandarini.

Alitoa agizo hilo jana wakati wa akizindua Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kuongoza Mkutano wa 10 wa Baraza hilo uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu, Dar es Salaam. “Kama alivyosema Waziri Mkuu, tunataka kufanyia kazi maoni yenu mara moja, kuanzia Jumatatu nataka taasisi zote za pale bandarini zitoe huduma saa 24, haiwezekani bandarini kwetu mizigo ichukue siku 13 kuitoa wakati bandari za wenzetu majirani inatoka baada ya siku tatu, tutashindana vipi?”
Alihoji Rais Magufuli. Rais alikuwa akijibu maoni ya wafanyabiashara hao ikiwemo tatizo la ucheleweshaji wa mizigo bandarini na hivyo kuagiza kuanzia kesho taasisi zote katika bandari ya Dar es Salaam na TPA kufanya kazi kwa saa 24.
Hata hivyo, Rais Magufuli aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji wajirekebishe kwa kasoro ambazo baadhi yao wanazo ikiwemo ukwepaji wa kodi, kupandisha viwango vya bei kwa huduma wanazotoa serikalini, kujihusisha na rushwa, kutaka faida kubwa isiyostahili bila kuwajali wananchi na kutochangamkia fursa za uwekezaji za ndani na nje ya nchi licha ya juhudi zake za kuwaleta viongozi na wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali.
“Nataka mjiulize amekuja Waziri Mkuu wa India, amekuja Rais wa Vietnam, amekuja Rais wa Uturuki, amekuja Rais wa Kongo (DRC), amekuja Rais wa Zambia, amekuja Rais wa Uganda, amekuja Mfalme wa Morocco na wengine wengi, tumenufaikaje? Mbona wao wanakuja kuwekeza hapa nyie kwa nini hamuendi kwao?” Alihoji.
Hata hivyo, Rais Magufuli aliwapongeza wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) inayoongozwa na Mwenyekiti wake Dk Reginald Mengi kwa juhudi kubwa zinafanywa kuendeleza biashara na uwekezaji nchini na kuahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwathamini na kushirikiana na wawekezaji na wafanyabiashara kwa manufaa ya Taifa.
Alieleza kufurahishwa na maoni, mapendekezo na dukuduku alizozipata kutoka kwenye mkutano huo na kuwahakikishia kuwa Serikali anayoiongoza itafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa ikiwemo kuondoa usumbufu unaosababishwa na uwingi wa taasisi zinazomhudumia na kumtoza mfanyabiashara na mwekezaji, kuongeza vivutio, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi mbalimbali na kuishirikisha sekta binafsi katika mipango na utekelezaji wa miradi.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa), Angelina Ngalula akitoa maoni ya sekta ya usafirishaji, pamoja na mambo mengine alilalamikia urasimu uliopo bandarini ambao unafanya mzigo kukaa bandarini siku kumi hadi 13 huku nchi nyingine wakitumia siku tatu hadi nne.
“Mwenyekiti vitu ambavyo vinatukwamisha ni pamoja na tunapoteza muda mwingi bandarini jambo ambalo linatufanya tukose ushindani, naipongeza TPA wameboresha huduma kwa sasa wanafanya kazi masaa 24 wengine hawafanyi wanatukwamisha,” alisema Angelina.
Alisema tatizo lililopo bandarini hakuna mratibu kuna taasisi nyingi ambazo pia zina mifumo yao huku wengine wafanyabiashara inabidi kuwafata katika ofisi zao ambazo hazipo bandarini. Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikiri kuwepo na urasimu mkubwa bandarini ambapo sekta ambazo zinafanya kazi zinakwamisha wafanyabiashara katika kutoa mizigo yao.
“Kuna urasimu wa hovyo sana bandarini, sekta ambazo hazifanyi kazi hatukubaliani nazo, kama TPA wanafanya kazi saa 24 kwanini TRA, TFDA, TBS, ningependa kupata taarifa Jumatatu kwamba hao wengine wanakesha sambamba na TPA,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Tanzania imelalamikiwa utendaji kazi wake katika bandari uko chini, alisema kama TPA wanafanya kazi saa 24 lakini mzigo utakwama kwa sababu taasisi hizo nyingine zinafanya kazi saa chache.
Alisema bandari ya Mombasa mzigo unachukua siku saba hadi nane kutoka bandarini wakati Bandari ya Dar es Salaam ni siku 13 ambapo alimtaka Waziri wa fedha ahakikishe TRA inafanya kazi saa 24.
Aliahidi wawakilishi wa sekta binafsi waliohudhuria mkutano huo kuwa Serikali itahakikisha maoni yao yote yanafanyiwa kazi ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali zake na kusonga mbele kimaendeleo.
“Naomba niwahakikishie kuwa hisia zenu tumezipata, maoni yenu tutayazingatia na tutahakikisha tunayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kwa pamoja tufanye kazi ya kuijenga nchi yetu,” alisema Majaliwa.
Wawakilishi wa sekta binafsi waliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi kubwa inazozifanya kujenga miundombinu muhimu kwa uwekezaji na biashara kama vile ujenzi wa reli, barabara, meli na ununuzi wa ndege, kukabiliana na rushwa, kusimamia mpango wa ujenzi wa viwanda, kujenga nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma na kujenga uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali duniani.
Miongoni mwa yaliyojitokeza katika kikao hicho ni kuiomba Serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika upangaji na utekelezaji wa mipango, sera na sheria mbalimbali za uwekezaji na biashara, kuendelea kuondoa vikwazo na urasimu ambao unachangia kupunguza ufanisi katika biashara na uwekezaji, kuongeza vivutio vya uwekezaji na kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi, utalii na viwanda.
Rais Magufuli akiwa mwenyekiti wa kikao hicho, alizindua pia Baraza la Tatu la Taifa la Biashara ambalo lina wajumbe 40, katika kikao hicho zaidi ya saa nne alizitumia kusikiliza maoni na changamoto za wafanyabiashara na baada ya hapo mawaziri kujibu hoja zinazowahusu kabla hajampa nafasi waziri mkuu na baadaye yeye kuzungumza.