Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania ya Halotel, Do Hong
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewatia hatiani, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania ya Viettel inayofanya biashara kama Halotel, Do Hong na wenzake wanane, kwa kosa la kuhujumu uchumi na kuwataka kulipa faini ya zaidi ya Sh. milioni 700.

Hata hivyo, Hong ameachiwa huru baada ya kulipa Sh milioni 479 ambazo kati yake, sh milioni 20 ni faini na sh milioni 459 ni fidia ya hasara anayodaiwa kuitia Serikali. Wenzake wamekwenda jela kwa kutolipa. Mbali ya Hong, washitakiwa wengine ni Dilshad Ahmed (36), Rohail Yaqoob (47), Khalid Mahmood (59), Ashfaq Ahmad (38), Muhamad Aneess (48), Imtiaz Ammar (33) wote raia wa Pakistan, Ramesh Kandasamy (36) raia wa Sri-Lanka na Viettel Tanzania Limited (Halotel) iliyoshitakiwa pia.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri alitoa hukumu hiyo jana baada ya washitakiwa hao kukiri makosa yao baada ya kusomewa upya mashitaka saba badala ya 10 waliyokuwa wameshitakiwa nayo kwa maelezo ya awali. Mashitaka waliyoshitakiwa nayo katika kesi hiyo ni kula njama kutenda kosa, kughushi na kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa. Hakimu Mashauri alisema katika kila kosa mshitakiwa atatakiwa kulipa Sh milioni tano na wanatakiwa kurudisha hasara yote walioisababishia serikali, ya Sh milioni 459.
“Washitakiwa hawa wamekuja kuwekeza nchini na lengo sio kuhujumu uchumi na miundombinu yetu. Ili iwe fundisho kwa wawekezaji wengine na kuonesha kwamba Tanzania ipo makini katika masuala haya, kila mshitakiwa atatakiwa kulipa Sh milioni tano na kuilipa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) fedha walizohujumu,” alisema Hakimu Mashauri katika hukumu. Pia Hakimu huyo aliagiza vifaa vyote walivyokutwa navyo washitakiwa wakifanyia biashara, vitaifishwe na serikali na akasema wanayo haki ya kukata rufaa Mahakama Kuu kuhusiana na adhabu pekee.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali, Jehovaness Zacharia, alidai hawana kumbukumbu ya makosa ya zamani ya washitakiwa hivyo mahakama iwape adhabu inayostahili kulingana na makosa. Katika mashitaka yao, inadaiwa kuwa kati ya Novemba 2016 na Februari 2017, Jijini Dar es Salaam, walitengenezamfumo wa kutumia huduma za mtandao kwa lengo la kukwepa kodi ya kupokea na kusambaza simu za kimataifa bila kibali cha TCRA. Pia wanadaiwa katika kipindi hicho waliendesha hiyo mifumo ya kupokea na kusambaza simu za kimataifa bila ya leseni.
Inadaiwa Novemba 20, 2016 waliingiza vifaa vya kielektroniki bila ya kuwa na leseni ambapo katika tarehe isiyofahamika Novemba 2016, walisimika vifaa hivyo ikiwamo sim box yenye namba ya siri 1152000.8.n.t.n na Laptop mbili aina ya Dell bila ya kuwa na kibali cha TCRA. Katika kipindi hicho, washtakiwa hao wanadaiwa kuunganisha vifaa hivyo na huduma za mitandao kwa lengo la kupokea na kusambaza mawasiliano bila ya kuthibitishwa na TCRA itakavyo sheria.
Viettel Tanzania Limited (Halotel) na Do Hong, wanadaiwa kati ya Novemba 2016 na Februari 2017 maeneo ya ofisi za Halotel Victoria Kinondoni, walishindwa kuthibitisha taarifa iliyotolewa na Unex Company Ltd kusajili laini za simu 1,000. Pia inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuisababishia hasara TCRA na serikali ya Tanzania ya Sh 459,000,000.