Rais wa Urusi Vladimir Putin ameingilia sakata inayomkabili Rais wa Marekani Donald Trump kutokana na uhusiano wake na Urusi.
Rais Putin amepinga madai ya uvujaji siri za Marekani kwa Urusi na kueleza kuwa yuko tayari kutoa kumbukumbu za mkutano wa viongozi hao kwa bunge na Seneti za Marekani ikihitajika.

Putin amesema kuwa mkutano haukufanyika unavyodhaniwa huku akitania hali hiyo.
"Nimezungumza na Lavrov, na nimemueleza sijafurahishwa naye kwa sababu amenificha siri," alisema.
Majarida mbalimbali ya Marekani yamefichua kuwa Rais Trump aliwapa viongozi wa Urusi taarifa kuhusu Islamic State ambazo zina uwezo wa kuhatarisha watoaji wa taarifa hizo.
Haya yanajiri huku taarifa zikienea kuwa Bw Trump alijaribu kushawishi uchunguzi unaoendelea kuhusu ushirikiano wa wawakilishi wake na Urusi.
Bwana Trump alikutana na waziri wa kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov na Balozi wa Urusi nchini Marekani Sergei Kislyak katika ikulu ya White house Jumatano, wiki iliyopita.
Mkutano huo unajiri wakati uchunguzi wa kuhusika kwa Urusi kwenye uchaguzi wa Marekani unaendeshwa na FBI na kupitia vikao maalum vya bunge za Marekani.
Taarifa hizo zilitajwa kuwa muhimu mno kiasi cha kutoenezwa kwa washirika wa Marekani wakiwemo Urusi wanaoshirikiana na wapinzani wa Marekani nchini Syria.
Hata hivyo Bw Trump alijitetea dhidi ya madai hayo huku mshauri wake usalama wa taifa, HR McMaster akiongeza vitendo vya rais vilikuwa sawa.