Katika hali isiyokuwa ya kawaida mtoto wa miaka 12, Dorcas Meshak mkazi wa kitongoji cha Mbughantigha kijiji cha Matongo tarafa ya Ikungi, ameuawa na watu wasiojulikana na kunyofolewa baadhi ya viungo vyake.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda Jeshi la Polisi mkoani hapa, SSP Isay Mbugh alisema Mei, 18 mwaka huu saa sita mchana wakati ambao Dorcas alipoondoka nyumbani kwao kwa lengo la kwenda shambani kuchuma mahindi, umbali wa kilometa 70.

Alisema mtoto huyo amenyofolewa macho yote mawili, kukatwa matiti yote na kuondolewa sehemu zake za siri.
“Mtoto Dorcas hakuweza kurudi nyumbani kitendo kilichosababisha ipigwe yowe ili watu wakusanyike kwa ajili ya kumtafuta. Haikuchukua muda mrefu, mwili wa Dorcas ulikutwa ukiwa umenyongwa hadi kufa kwa kamba ya ngozi,” alisema.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mauaji hayo yanahusishwa na imani za ushirikina na hadi sasa hakuna watu waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo.
Katika tukio la pili, Kaimu Kamanda Mbugh, alisema watu wawili wamepoteza maisha kufuatia kutokea ajali ya gari anina ya Noah, tukio ambalo lilitokea Mei, 20 mwaka huu saa 6.45 mchana huko katika kijiji cha Mwaja tarafa ya Unyankumi Manispaa ya Singida.
“Ajali hiyo imehusisha noah T.402 DFH iliyokuwa ikiendeshwa na Said Shaban (33), na chanzo cha ajali ni mwendo kasi kitendo kilichosababisha ashindwe kulimudu. Waliofariki kwenye ajali hiyo,ni Elia Daniel (34) mkulima kijiji cha Mwankoko na mwanamke mmoja ambaye jina wala makazi yake,hayajafahamika,” alisema.
Aidha, aliwataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Mratibu Elimu kata ya Mtamaa, Nicodem Elias (45), Juma Ramadhan, mwalimu Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Elia Bilau mkulima na mkazi wa Magungumka Kapela Donad (28).
Kaimu kamanda huyo, alisema dereva wa Noah hiyo Said Shaban anashikiliwa na Jeshi la Polisi na upepelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.