Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea kwa huzuni na masikitiko  makubwa taarifa ya vifo vya watoto 32, walimu 2 na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent ya Arusha, vilivyosababishwa na ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu - Arusha. 

Tunasikitika sana kwa kuwa ajali hii imetokea wakati wazazi, walezi na walimu wakitekeleza wajibu wao wa msingi wa kumpatia mtoto haki ya kuendelezwa Kielimu.

Kufuatia msiba huu mkubwa, kwa niaba ya Wizara na kwa niaba yangu mwenyewe ninatoa pole kwa wazazi, walezi, familia na jamii yote ya Arusha na Tanzania kwa ujumla, kwa kupoteza watoto wetu ambao walikuwa wanaandaliwa kuwa nguvu kazi ya Taifa letu katika Sekta mbalimbali. Tunamuomba 

Mwenyezi Mungu awapatie Faraja na Moyo wa Subira  katika kipindi hiki kigumu cha huzuni, uchungu na simanzi kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla. 

Tunaziombea roho za watoto wetu wapendwa zipumzishwe mahali pema peponi, Amiin. Ni maombi yetu pia kuwa Majeruhi waliopo hospitalini watapata nafuu ili waweze kuendelea na masomo.

Ummy Mwalimu, Mb

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

07/05/2017