Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni, wametia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba ambao utasainiwa baadaye kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

Hafla ya kutia saini tamko hilo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Wakurugenzi na Viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.
Baada ya kutia saini tamko hilo, wataalamu wataandaa mkataba wa mradi kati Tanzania na Uganda ambao umepangwa kukamilika katika kipindi cha wiki moja, na baada ya hapo taratibu za kuweka jiwe la msingi la kwanza kwa ujenzi wa mradi huo zitafanyika.
Ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Hoima -Tanga wenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,443 zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania utagharimu Dola za Marekani Bilioni 3.55, unatarajiwa kusafirisha mapipa laki 2 ya mafuta kwa siku na wakati wa ujenzi unatarajiwa kuzalisha ajira kati ya 6,000 na 10,000.
Akizungumza baada ya kutia saini tamko hilo Rais Magufuli amemshukuru rais Museveni kwa hatua ambayo Tanzania na Uganda zimefikia katika mradi wa bomba la mafuta na ameeleza kuwa mradi huo ni matokeo ya urafiki na udugu wa kihistoria ulioko kati ya nchi hizi mbili.
Rais Magufuli amesema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Uganda, Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika nzima, na kwamba pamoja na faida zilizoainishwa kwa bomba hilo kupitia Tanzania ni uwepo wa amani, uzoefu wa Tanzania katika uendeshaji wa miradi ya mabomba ya mafuta na gesi, jiografia nzuri ya usafirishaji mafuta, ardhi na ubora wa bandari ya Tanga, Tanzania inaupokea mradi huo kwa heshima kubwa na ni kumbukumbuku kubwa ya Rais Museveni na Serikali yake.
"Huu ni mradi mkubwa sana, najua Uganda mmepata mapipa Bilioni 6.5 ya mafuta huko Hoima na pengine mtapata mengine na sisi pia tunatarajia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, haya yote tutayapitisha kwenye bomba hili hili.
"Kwa hiyo mimi nakushukuru sana rais Museveni na kwa niaba ya Watanzania wote tumefurahi sana, umetengeneza historia ya Tanzania na Uganda na pia umeimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu, Watanzania hawatakusahau" amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake rais Museveni amempongeza rais Magufuli na Serikali yake kwa kutia msukumo mkubwa kufanikisha mradi huu na amesema mradi huu utazinufaisha nchi za Afrika Mashariki yakiwemo mashirika ya ndege ambayo yatapata mafuta kwa gharama nafuu na hivyo kukua zaidi kibiashara.
Rais Museveni ameuelezea mradi huo kama moja ya matokeo ya ushirikiano na ametoa wito kwa viongozi hasa vijana kuendeleza misingi ya umoja na ushirikiano kati ya nchi zao ili kujipatia manufaa ya kiuchumi."Nimefurahi sana leo, najua kuna kazi kubwa imefanyika hadi kufikia hatua hii, lakini hii pia imeonesha kuwa na sisi tunaweza" amesema rais Museveni.