WABUNGE wametoa kilio chao kutokana na sekta ya afya nchini kuathirika zaidi kutokana na idadi kubwa ya watumishi wengi waliotumbuliwa baada ya kubainika kuwa na vyeti feki kutokea katika sekta hiyo muhimu kwa maisha ya watu.

Aprili 28, mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki yenye majina ya watumishi 9,932 kutoka sekta mbalimbali, ikiwamo ya afya ambao walibainika kuwa na vyeti feki vya kidato cha nne na cha sita na vile vya ualimu.
Kutokana na orodha hiyo iliyohusisha watumishi kutoka Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na Ofisi ya Rais Utumishi, imewagusa watumishi wa sekta ya afya katika hospitali, vituo vya afya na hasa kwenye zahanati.
Kutokana na sekta hiyo kuhusisha afya ya maisha ya watu, wabunge wameiomba serikali ichukue hatua za makusudi kuziba nafasi za watumishi wa afya ambao wengi wametumbuliwa kutokana na kutumia vyeti feki katika ajira yao.
Juzi, Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro aliwaambia waandishi wa habari kwamba serikali itajaza nafasi hizo haraka sana hasa katika maeneo ambayo yameathiriwa sana na kuondoka kwa watumishi hao walioghushi vyeti ambao wametakiwa kuondoka kwa hiari yao kabla ya Mei 15, mwaka huu vinginevyo watakabiliwa na mashitaka ambayo ukitiwa hatiani adhabu yake ni kifungo cha miaka saba jela.
Akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto bungeni jana, Mbunge wa Mchinga, Hamid Bobali (CUF) alisema katika jimbo lake, zahanati mbili zimefungwa kutokana na wafanyakazi wake kutumbuliwa kutokana na kutumia vyeti feki.
Bobali alisema serikali inatakiwa kufanya jitihada kunusuru afya za wananchi wa maeneo hayo kutokana na kukosa huduma ya afya kutokana na wafanyakazi wake kutumbuliwa. Alisema licha ya Jimbo na Mkoa wa Lindi kuwa na watumishi wa kada ya udaktari wachache, kutumbuliwa kwa wafanyakazi hao kumechangia kuathiri huduma za afya zaidi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Lathifar Chande (Chadema) alisema kutokana na tumbua tumbua wafanyakazi wa afya wamepungua na hivyo kuzorotesha huduma za afya katika Hospitali ya Mkoa ya Lindi.
“Wauguzi wamepungua kutokana na tumbua tumbua ya vyeti feki, hao wachache walikuwa wamebaki na kusababisha kuzorotesha huduma hiyo,” alisema Chande. Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Jasmin Bunga (CCM) alisema serikali inatakiwa kuboresha vyuo vya maendeleo ya jamii ili kuhakikisha watumishi wanapatikana wa kutosha wa kutoa huduma hiyo.
“Vyuo vya ustawi wa jamii ndio injini, inatakiwa kuboresha vyuo hivyo mfano cha Tengeru ili kutoa watumishi ambao watachangia katika kutoa huduma bora kwa jamii,” alisema mbunge huyo.