Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven
KATIKA kuhakikisha anakomesha tatizo la ujauzito kwa wanafunzi, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha ndani ya siku saba inazifikisha mahakamani kesi 50 za wanafunzi waliopewa ujauzito wilayani humo.

Amesisitiza kuwa, wasichana waliobeba ujauzito lazima washitakiwe ili waweze kuwataja wanaume waliohusika. Aidha, amewapa siku saba watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wazazi wa watoto 200 ambao hawajaripoti shuleni kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu, wanakamatwa na kufikishwa kortini.
Alitoa maagizo hayo wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa wilaya ya Nkasi kilichoketi jana mjini Namanyere yalipo makao makuu ya wilaya ya Nkasi. “Hali hii haiwezi kuvumilika hapa mjini Namanyere peke yake kuna zaidi ya wasichana 30 ambao wamekatiza masomo yao baada ya kupatiwa ujauzito huku katika Kituo cha Polisi cha wilaya ya Nkasi kuna mashauri ya wanafunzi wa kike 50 ambao wamepewa ujauzito, lakini bado hayajafikishwa mahakamani.
“Nasema sio kazi ya polisi kusuluhisha kesi za wanafunzi waliopewa ujauzito , tutakitafiti kituo hiki cha polisi maana zipo taarifa kinachofanyika pale wana bargain (jadiliana ili kumaliza kesi kienyeji) na unasikia mtuhumiwa ametoroka.
Sasa, naagiza kesi zote hizo zifikishwe mahakamani ndani ya siku saba,” alisema. Mkuu huyo wa wilaya ambaye ni mbunge wa zamani wa Jimbo la Nchinga mkoani Lindi, pia ameyaagiza mabaraza ya kata yawe yamemaliza kusikiliza mashauri ya kesi za mimba kwa wanafunzi ndani ya siku saba na hatua zichukuliwe.
Aliwashangaa madiwani wa halmashauri hiyo katika taarifa zao walizowasilisha kwani hazikuonesha idadi ya wanafunzi waliopewa ujauzito wala wale ambao hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza katika shule za umma tangu zifunguliwe mapema mwaka huu .
“Leo mkiulizwa katika baraza hili mna maazimio yapi hakuna katika mijadala yenu kinachosikika ni taarifa miongozo na kanuni,” alisema. Wakichangia baadhi ya madiwani waliishauri Serikali iwapatie semina elekezi watendaji wa mabaraza ya kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.