Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete jana aliwaongoza mamia ya wakazi wa Dar es Salaam, kuuaga mwili wa aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu anayetarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Malinyi, mkoani Morogoro.

Aidha, mwanahabari nguli aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kwanza wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Paul Sozigwa ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kwanza wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), anatarajiwa kuzikwa Jumanne nyumbani kwao Kisarawe, mkoani Pwani.
Mwambungu na Sozigwa waliaga dunia juzi kwa nyakati tofauti Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) walikokuwa wamelazwa. Mwambungu aagwa Mwili wa Mwambungu uliagwa jana nyumbani kwake Tabata Kimanga, Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda Malinyi anakotarajiwa kuzikwa leo saa 10 jioni.
Akizungumzia chanzo cha kifo cha Mwambungu, mtoto wa kwanza wa marehemu, Hamidu Mwambungu alisema, baba yake alikuwa akisumbuliwa na figo na Saratani ya damu iliyokuwa ikishambulia mifupa. Kabla ya kukimbizwa JKCI Jumatano, aliwahi kulazwa India kwa miezi mitatu na afya yake iliimarika kwa muda.
Sozigwa kuzikwa Jumanne Sozigwa ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi katika Serikali ya Awamu ya Kwanza anatarajiwa kuzikwa keshokutwa katika makaburi ya Mission yaliyopo Kisarawe mkoa wa Pwani.
Mpwa wa Sozigwa, Mchungaji Mwipile Ismail aliliambia gazeti hili kuwa, Sozigwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu ambalo madaktari walisema lilisababishwa na kufanya kazi nyingi bila kupumzika.
“Hii inaweza kuwa ni kweli kwa sababu wakati wote mzee alikuwa akifanya kazi sana, alikuwa hapumziki, lakini pia baadae akawa na tatizo la moyo na baadae tena madaktari walibaini kuwa alikuwa na saratani,” alisema Mchungaji Ismail.
Kwa mujibu wa Mchungaji Ismail, kesho mchana mwili wa Sozigwa utafanyiwa ibada katika Kanisa la Kiinjili na Kilutheri (KKKT), Usharika wa Mtoni na mwili utasafirishwa Jumanne asubuhi kwenda Kisarawe kwa ajili ya mazishi.