Kiungo mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard atakosa mwanzo wa msimu ujao Ligi ya Premia baada yake kufanyiwa upasuaji kwenye kifungo cha mguu.

Hazard, 26, amekuwa akihusishwa na kuhamia Real Madrid.
Aliumia kwenye mfupa kifundo cha mguu wa kulia akifanya mazoezi akiwa an timu ya taifa ya Ubelgiji Jumapili.
Chelsea walisema upasuaji huyo aliofanyiwa Jumatatu ulienda vyema na kwamba anatarajiwa kukaa kwa miezi mitatu kabla ya kuanza kufanya mazoezi.
Msimu mpya Ligi ya Premia utaanza mnamo 12 Agosti.
Hazard pia atakosa mechi za kabla ya msimu dhidi ya Arsenal, Bayern Munich na Inter Milan nchini Singapore kati ya 22-29 Julai, na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal mnamo tarehe 6 Agosti.
Hazard aliwasaidia sana Chelsea kushinda Ligi ya Premia msimu uliomalizika majuzi ambapo aliwafungia mabao 16 katika mechi 36.
Hazard alipakia picha kwenye Twitter akiwa hospitalini na kuandika: "Kila kitu kilikwenda vyema kuhusu upasuaji wangu kifundo cha mguu, na saa naanza safari ya kuelekea kupata nafuu! Nitakuwa na nguvu zaidi. Asanteni kwa uungaji mkono wenu!!"