Wananchi wilayani Handeni wapigwa marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji na kutakiwa kutunza mazingira ili kuwezesha uendelevu wa maisha.
Marufuku hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika ngazi ya wilaya katika Kata ya Mkata katika bwawa la Tulafimbo.
Gondwe alisema kuwa wananchi lazima wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60. “Kwa kuzingatia sheria hiyo, kupiga marufuku kwa wananchi kufanya shughuli zozote za kibinadamu zenye kuhatarisha usalama wa maji na uchafuzi wa mazingira kwenye maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji wilayani Handeni” alisema Gondwe.
Aidha, aliwataka maafisa Tarafa, maafisa watendaji wa Kata na wenyeviti wa Vijiji kuhakikisha wanatengeneza mipaka kwenye maeneo ya vyanzo vya maji vyote vilivyopo Wilayani Handeni msimu huu ambao mvua imenyesha ya kutosha na vyanzo vingi vimejaa maji. “Hii itasaidia kuzuia uvamizi wa maeneo hayo na kurahisisha kuchukua hatua kwa watu watakaokwenda kinyume na amri hiyo” alisema Gondwe.
Gondwe, aliwataka wananchi wote walionunua mashamba kwa lengo la kilimo kusafisha mashamba yao kwa kuacha asilimia 30 ya uoto wa asili badala ya kusafisha maeneo yote ambayo wamenunua. “Tusipotunza mazingira, itakuwa ni ubinafsi kwa kizazi chetu na kizazi kijacho. Tukitendee haki kizazi hiki na kijacho kwa kuondoa ubinafsi wa kuharibu mazingira” alisema Gondwe.
Wakati huohuo, aliwataka viongozi ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji kutunza kutunza mazingira kwa kusimamia uwiano wa ardhi uliyopo na idadi ya mifugo ili kutunza mazingira kwa kuwa na mifugo inayoendana na rasilimali ardhi iliyopo. Aliwataka kuweka mikakati ya kupiga chapa mifugo ili kurahisisha utambuzi wa mifugo hiyo wilayani Handeni.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Makufwe aliwataka wananchi kutunza rasilimali maji kidogo inayopatikana kwa kipindi cha mvua kwa kupanda miti kwenye maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji. Alisema kuwa Serikali inaendelea kushughulikia changamoto ya upatikanaji maji ya kudumu Wilayani Handeni.
Aliwataka wakuu wa shule za msingi na sekondari kuhakikisha kila mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza hadi la saba na kidato cha kwanza hadi cha nne anakuwa na mti wake anaoutunza ili anapomaliza shule akikabidhiwa cheti na yeye akabidhi mti alioutunza kwa kipindi chote alichokuwa shuleni.
Maadhimisho ya wiki ya mazingira kiwilaya yalitanguliwa na upandaji miti 28,954 yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “hifadhi ya mazingira muhimili kwa Tanzania ya viwanda”.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akipanda mti kwenye maadhimisho.
Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe iyeshika chepeo na mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mh Ramadhani Diliwa wakipanda mti.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akizungumza na wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe akizungumza na wananchi wakati wa maadhimisho.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh Ramadhani Diliwa akizungumza na wananchi.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mkata wkisherehesha kwa Ujumbe wa utunzaji mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe iyeshika chepeo na mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mh Ramadhani Diliwa wakipanda mti.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akizungumza na wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe akizungumza na wananchi wakati wa maadhimisho.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh Ramadhani Diliwa akizungumza na wananchi.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mkata wkisherehesha kwa Ujumbe wa utunzaji mazingira.
0 Comments