Familia ya Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama imenunua nyumba ambayo kwa muda wamekuwa wakiishi kwa kukodisha mjini Washington DC.
Nyumba hiyo yenye vyumba tisa inapatikana katika mtaa wa kifahari wa Kalorama na iliuzwa $8.1m (£6.2m).

Obama ameamua kuendelea kukaa Washington na familia yake hadi binti yake mdogo, Sasha ambaye ana umri wa miaka 15, amalize masomo ya shule ya upili.
Kiongozi huyo na mkewe Michelle wamekuwa wakizuru mataifa mbalimbali duniani tangu walipoondoka White House mwezi Januari.
Msemaji wa Bw Obama, Kevin Lewis, alithibitisha ununuzi huo na kusema: "Ikizingatiwa kwamba Rais na Bi Obama watakuwa Washington kwa angalau miaka mingine miwili unusu, ina umuhimu kwao kununua nyumba badala ya kuendelea kukodi."
Kuna vizuizi vya saruji kuzuia watu kufikia nyumba hiyo yenye ukubwa wa futi mraba 8,300 (mita mraba 770), ambayo inalindwa saa 24 kila siku na maafisa wa kikosi cha kulinda marais Marekani.Familia ya Obama bado inamiliki nyumba Chicago.
Walinunua nyumba hiyo kutoka kwa aliyekuwa afisa wa habari wa Bill Clinton Joe Lockhart, aliyeinunua mwaka 2014 kwa $5.3m.
Nyumba hiyo haiko mbali sana na nyumba ya thamani ya $23m inayomilikiwa na mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos, ambaye pia humiliki gazeti la Washington Post.
Bintiye Rais Donald Trump, Ivanka, na mumewe Jared Kushner ambaye kwa sasa ni mshauri mkuu White House, pia wanaishi hapo karibu.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson ni afisa mwingine wa ngazi ya juu anayeishi Kalorama, katika nyumba aliyoinunua kwa $5.6m Februari.