Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi hiyo.
Bw Majaliwa amesema yeyote atakayekamatwa akijaribu kusafirisha chakula nje ya nchi hiyo, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la taifa.
Akiongea wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid, waziri mkuu huyo alisema serikali imechukua hatua hiyo kuzuia Tanzania isikumbwe na baa la njaa.
"Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini," amesema.
"Jana nimeona kwenye televisheni taarifa kuhusu malori 10 yaliyokamatwa Tarakea yakiwa na mahindi tayari kuvushwa mpaka. Mheshimiwa RC akasema chakula hicho ni lazima yarudishwe kwa ajili ya usagaji."
"Mimi nasema kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa."
Bw Majaliwa amesema kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila kibali.
"Hilo ni kosa kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu kupata baa la njaa huko mbele," amesema.
Amesema mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari imekuwa inapitisha kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jambo ambalo ni hatari sana.
"Hii ni kwa sababu chakula cha ndani hakitoshelezi mahitaji. Kwa sababu nchi zote za jirani hazina chakula cha kutosha. Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia njaa."
Kenya ni moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na uhaba wa mahindi.
Bw Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa ndani, wachukue mahindi kutoka maeneo yenye mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu zenye mavuno kidogo.
"Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe huku kwenye mavuno mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako wanayahitaji au tukanunue Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine yenye upungufu," alisisitiza.
|
0 Comments