Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
BAADHI ya wabunge wameitaka serikali kufanya maamuzi magumu pamoja na kutoa adhabu ya kunyonga kwa watendaji wote wa serikali, waliohusika na mikataba mibovu, iliyosababishia taifa kuibiwa makinikia kwa muda mrefu.
Aidha wabunge hao wameitaka Serikali, iwasilishe bungeni mikataba yote ili iweze kupitiwa na itakayokutwa na makosa irekebishwe, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama na rasilimali zao.

Mbunge wa Nkasi, Ally Keissy, ndiye aliyeanza kuibua hoja ya watendaji hao kunyongwa wakati akichangia kwenye mjadala wa Kamati ya Matumizi ya Bunge ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema wakati umefika sasa wa kufukua makaburi, kwa kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na mikataba mibovu, ambayo kutokana na kuthubutu kwa Rais John Magufuli, tume aliyoiunda iliweza kubaini madudu ikiwemo kuibiwa kwa kiasi kikubwa cha madini ya dhahabu.
“Sasa hivi hali imekuwa mbaya, wananchi wanataabika, viongozi wanagombana kwa sababu ya watu wachache hivyo ni bora wachukuliwe hatua na ikiwezekana wanyongwe kwa kulisaliti taifa lao,” alisisitiza.
Mbunge huyo alitishia kushika shilingi ya mshahara wa waziri hadi pale atakapothibitishiwa na serikali kuwa watendaji na wahusika wote wa mikataba hiyo mibovu, watachukuliwa hatua ikiwemo kunyongwa.
Kwa upande wake, mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel (CCM) aliunga mkono hoja hiyo ya Keissy na kuishauri serikali kuwasilisha mikataba yote bungeni, iweze kupitiwa ili kuondoa mapungufu ambayo bado yanayoendelea kulitafuna taifa.
“Nakubaliana na hoja ya Kessy kwamba kwa sasa Tanzania tunahitaji mikataba yote kupitiwa upya, na nina matumaini kuwa kwa hili tutafanikiwa kwani tayari rais ameonyesha dira,” alisema.
Naye mbunge wa Bukene, Selemani Zedi (CCM), alisema pamoja na kuiunga mkono hoja ya Keissy ni wakati muafaka sasa wa Bunge hilo kuanza kuipitia mikataba yote kutokana na ukweli kuwa bado mikataba mingi, ina maeneo yanayohitaji kurekebishwa kwa manufaa ya Watanzania.
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), alisema Watanzania wameteseka kwa muda mrefu na nchi yao kufanywa shamba la bibi kutokana na kuibiwa rasilimali zao, hasa madini.
“Mimi namuunga mkono Keissy katika hili, tufanye maamuzi magumu hata kama wahusika wasiponyongwa, lakini wachukuliwe hatua kali, pia na hii mikataba iletwe bungeni tuijadili na kupitia,” alieleza.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema pamoja na kwamba waliohusika wameliingiza taifa katika hasara kubwa, kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba, zipo hatua kali za kisheria wanazoweza kuchukuliwa.
Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, zipo taratibu zilizotafsiriwa kisheria zinazoelezea makosa yanayosababisha mkosaji kunyongwa. “Makosa haya ya kupoteza rasilimali zetu pia yanaweza kutafutiwa adhabu kali kwa mfano kwa sasa tuna mahakama ya ufisadi. Lakini hili la kunyongwa lazima tufuate sheria zinavyosema,” alisema.
Naibu wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, alisema suala la kunyongwa ni la kijinai, ila tayari Rais ameunda kamati nyingine kwa ajili kuangalia suala hilo kisera na kisheria na itatoa mapendekezo yake hivi karibuni.
Mjadala ACT wanasiasa na wataalamu wakizungumzia mikataba ya madini wametaka umakini katika mabadiliko ya sheria za madini na mikataba ya kimataifa pamoja kuwapo kwa haja ya kutumia mifumo ya malipo ya kimataifa kwenye migodi ili kunufaika nayo.
Aidha, wameeleza iko haja ya kujifunza kutoka kwa nchi kama Botswana, ambayo ilifanya mabadiliko makubwa kwa kukaa chini na kujadiliana na hatimaye kuanza kunufaika na rasilimali ya madini ya almasi.
Hayo yalielezwa jana katika Kongamano la Rasilimali Madini, lililoandaliwa na chama cha ACT Wazalendo, ambalo lilikuwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya madini ikiwemo suala la makinikia linaloendelea kwa sasa.
Akizungumza katika kongamano hilo, Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alisema, lengo la kongamano hilo ni kwenda katika mjadala na mapana yake kisha kupata majibu ya namna gani ya kwenda mbele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa timu ya Wanasheria na Watetezi wa Mazingira (LEAT), Dk Rugemeleza Nshala alisema iko haja ya sheria za madini kubadilishwa, lakini zibadilishwe kwa majadiliano makubwa ya kushirikisha wadau mbalimbali.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa migodini (NUMET), Nidomedes Kajungu alisema matatizo mengi katika sekta ya madini yametokana na usiri wa mikataba. Alisema ni vyema serikali ikatunga sheria itakayowapa mamlaka wananchi kusimamia mali yao na kuwapa umiliki wa milele wananchi.
Bavicha wasema
Nalo Braza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeiomba serikali kuweka wazi mikataba yote ya gesi, madini na uwindaji wa wanyamapori. Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi alisema hayo jana kwenye mkutano na waandishi wa habari.
“Cha msingi la kufanya ni kuiweka mikataba hii hadharani ili tujue nini kinachojiri katika matumizi endelevu ya rasilimali za taifa letu, “ alisema Patrobas. Imeandikwa na Halima Mlacha, Dodoma; Katuma Masamba na Regina Mpogolo, Dar.