RAIS John Magufuli amemteua Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, ilisema Mghwira anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Saidi Meck Sadiki aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo.
Pia, taarifa hiyo ilisema kuwa Rais Magufuli amemteua Meja Jenerali Issah Suleiman Nassor kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi huo, Meja Jenerali Issah Suleiman Nassor alikuwa Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ). Hali kadhalika, Rais Magufuli amemteua Abdulrahman Kaniki kuwa Balozi.
Kabla ya uteuzi huo, Kaniki alikuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (DIGP). Tarehe ya kuapishwa kwa wateule wote itatangazwa baadaye, ilimalizia taarifa hiyo. Mghwira ni nani?
Anna Mghwira ni msomi mwenye shahada tatu na kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, ambacho Kiongozi wao Mkuu ni Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini.
Alikuwa mmoja wa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Mghwira alizaliwa mwaka 1959 mjini Singida na elimu ya sekondari aliipata katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Ihanja mkoani humo na kuhitimu mwaka 1978.
Mwaka 1981 alihitimu kidato cha sita katika Seminari ya Lutheran Junior iliyopo mjini Morogoro. Kisha alijiunga na Chuo Kikuu cha Tumani na kutunukiwa Shahada ya Theolojia. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisomea Sheria na kutunukiwa Shahada ya Sheria.
Pia ana Shahada ya Uzamili ya Sheria aliyoipata nchini Uingereza mwaka 2000. Alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwaka 2009 ambako aliwahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake ngazi ya wilaya na kisha Katibu wa Wanawake ngazi ya Mkoa.
Kuhusu Kaniki Kaniki alijiunga na Jeshi la Polisi Dar es Salaam mnamo Agosti 1990 na kuhitimu Januari 1991, ambapo alipata mafunzo ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi. Baadhi ya vyeo ambavyo amewahi kushika akiwa ndani ya jeshi hilo ni Mkaguzi wa Polisi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Mrakibu wa Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Naibu Kamishna na Kamishna.
Pia Kaniki, ambaye amesomea taaluma ya sheria, amewahi kufanya kazi kama Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi Dar es Salaam, Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Utafiti na Kamishna wa Uchunguzi wa Sayansi ya Makosa ya Jinai
|
0 Comments