Na
Tamimu Adam - Jeshi la Polisi


Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwaua watu
wawili  wanaosadikiwa kuwa  ni miongoni mwa wahalifu wanaoendesha mauaji
katika  Kanda maalumu ya  kipolisi Rufiji ambapo  mmoja  kati ya watu hao  ametambulika  kwa jina la Abdallah Ally Ngande Makeo ambaye
alikuwa anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa muda mrefu kutokana na kushiriki  kwake katika matukio ya  mauaji maeneo ya Ikwiriri, Kibiti pamoja na
uvamizi wa kituo cha Polisi Ikwiriri.

Akielezea tukio hilo,
Mkuu wa Operesheni Maalum  za
Jeshi la Polisi,  Naibu Kamishna wa
Polisi Liberatus Sabas alisema kuwa tukio hilo lilitokea mnamo tarehe 19,
julai, 2017 saa mbili usiku katika eneo la
Utende kata ya Ikwiriri,  wilaya Rufiji
kanda maalum  ya Polisi  Rufiji.

 “Askari  Polisi  wa doria
waliwatilia mashaka watu wanaokadiliwa kuwa watano ambapo walipoanza
kuwafutilia ndipo walianza kukimbia huku wakiwashambulia  askari kwa risasi. Askari nao kwa ujasiri walijibu
  mashambulizi na kufanikiwa  kuwajeruhi
wahalifu wawili miongonio mwao ambao baadaye  walifariki
wakipelekwa Hospitali  ya Taifa ya
muhimbili kutokana na kuvuja damu iliyosababisishwa na majeraha ya risasi
waliyoyapata” alisema Sabas.


Aliongeza kuwa  katika eneo
hilo la tukio ilipatikana silaha moja aina ya rifle 375 ambayo  ilikutwa imekatwa kitako na mtutu ikiwa na
risasi mbili (2).  Aidha, Miili ya
marehemu wote wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya
Taifa ya muhimbili. 


 Kamanda sabas
ameendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi
katika kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa wahalifu wengine waliosalia na
kwamba  opereheni hiyo ya kuwasaka
wahalifu katika Kanda hiyo ya kipolisi Rufiji
ni endelevu  na hakuna atakayebaki.