Rais mstaafu Benjamin Mkapa
RAIS John Magufuli na Rais mstaafu Benjamin Mkapa jana mara baada ya kukutana jukwaani, kila mmoja kwa wakati wake alianza kumwagia sifa mwenzake, huku Dk Magufuli akimshukuru Mkapa kwa kumuona na kumpatia nafasi ya uongozi.

Hali hiyo ilijitokeza kwenye Uwanja wa Mazaina wilayani Chato mkoani Geita katika sherehe za kukabidhi nyumba 50 kwa ajili ya mikoa mitatu ambayo ni Geita, Simiyu na Kagera za watumishi wa afya zilizojengwa na Taasisi ya Benjamin William Mkapa chini ya ufadhili wa Taasisi ya Mfuko wa Kimataifa Dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund).
Wakati akizungumza katika sherehe hizo, Mkapa alimpongeza Dk Magufuli kwa utendaji wake na kuelezea namna alivyomuibua na kumpatia uongozi wa juu akianzia na nafasi ya Unaibu Waziri. “Wakazi wa Chato ningewaomba msijivunie tu kwa Chato kupandishwa hadhi na kuwa wilaya, jivunieni kwa wilaya hii kutoa Rais wa nchi anayekubalika nchini kwake na dunia kwa ujumla,” alisema Mkapa.
Alisema wakati alipokuwa Rais wa Awamu ya Tatu, alimteua Dk Magufuli kuwa Naibu Waziri kutokana na utendaji wake na kwamba Chato ilikuwa ni moja ya maeneo yaliyokuwa yakifanya vizuri kwa wakati huo. Alisema kitendo cha kumuibua Rais huyo, sasa ni mmoja wa viongozi wanaosifika duniani kwa utendaji kazi na uchapakazi unaonekana na kuwataka wananchi wamsaidie kwa kumtanguliza Mungu.
Aidha, alitumia fursa hiyo kubainisha wazi kuwa kwa upande wake alichostaafu ni nafasi ya urais, lakini hajastaafu siasa kwani yeye ni mwanachama wa CCM nafasi ambayo atakuwa nayo hadi mwisho wa maisha yake. Katika kurudia kile alichokisema Jangwani katika kipindi cha kampeni mwaka 2015, Rais huyo mstaafu alipongeza kazi inayofanywa na serikali katika sekta ya afya na kubainisha kuwa kutokana na takwimu za maendeleo katika sekta ya afya, ni wazi kuwa zitapunguza kidogo kiwango cha upumbavu.
“Wale niliowaita malofa na wapumbavu naamini maendeleo haya katika sekta ya afya, yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa upumbavu wao,” alisema Mkapa. Katika mkutano huo wa Jangwani, Rais Mkapa alizua mjadala baada ya kutamka hadharani kuwa wanaotaka kuikomboa Tanzania ni malofa na wapumbavu kwani tayari nchi hiyo ilishakombolewa tangu mwaka 1961.
Naye Dk Magufuli pamoja na kubainisha kuwa alihudhuria sherehe hizo kama mwalikwa na si mgeni rasmi alimshukuru Rais Mkapa kwa kumteua kuwa kiongozi katika utawala wake, huku akikumbushia namna Rais huyo alivyomwombea kura za ubunge kipindi hicho. “Katika uwanja huu (Mazaina Chato), ulinisimamisha na kuniombea kura na hata baada ya hapo, uliniteua na kuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri. Nakushukuru sana, najua hupendi sifa ila kwa hili nitampa hata Mama Mkapa kutokana na kukushauri vizuri,” alieleza.
Pamoja na hayo, alibainisha kuwa yeye ni Rais anayefahamu vyema maisha halisi ya Watanzania kwani alipitia maisha ya umasikini ikiwemo kuuza maziwa na kuchunga ng’ombe. “Ndio maana mimi leo hii ni Rais mtetezi wa wanyonge, nafahamu vyema maisha ya Watanzania, na wengi wao ni masikini, sitaki waonewe. Ninamuomba Mungu aniondolee kiburi nisisahau nilipotoka,” alisema Dk Magufuli.
Mwaka 1995 baada ya kushinda ubunge jimbo la Biharamulo Magharibi wakati huo, Rais Mkapa kwa mara ya kwanza alimteua Dk Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na baadaye baada ya uchaguzi mwaka 2000, alimteua kuwa Waziri kamili wa wizara hiyo