Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Ally Hapi alimeliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kumkamata Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (pichani) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa tuhuma za kutoa lugha za matusi, dhihaka na uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Hapi alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake jana, na kuongeza kuwa wilaya yake si ya kuchezewa na wanasiasa kwa kutoa maneno ya kejeli dhidi ya rais na viongozi wengine wa serikali.
Alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, anataka mbunge huyo akamatwe na kuhojiwa kwa saa 48 pamoja na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. “Namtaka Halima akae saa 48 korokoroni ili aweze kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili aeleze hayo aliyoyasema yapo sawa kisheria,” alieleza Hapi. Akitoa agizo hilo, alisema Mdee anatakiwa kutafutwa na kukamatwa kisha kuwekwa rumande kwa saa 48 pamoja na kuhojiwa sababu za kutaka kuvuruga usalama.
Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema hadi jana jioni saa 11 kasoro robo walikuwa hawajamkamata Mdee na wanamtafuta. “Nimetoa agizo hili kutokana na hatua ya mbunge huyu wa Kawe kwa tiketi ya Chadema, kufanya mkutano wa wanahabari Makao Makuu ya chama hicho jana (juzi) jijini Dar es Salaam na kutoa maneno yasiyo ya kiungwana.
“Sitamvumilia mwanasiasa yeyote atakayethubutu kutoa kauli za matusi dhidi ya mheshimiwa Rais, au zenye kutaka kuleta uchochezi katika wilaya yangu,” alibainisha Hapi. Alisema kitendo cha Mdee kumwambia Rais Magufuli kuwa ana tabia za ovyo, ni kosa kubwa kisheria kwa kutoa maneno hayo kwa kiongozi wa nchi, ambaye alichaguliwa kwa kura za wananchi.
Alisema Ibara ya 33 ya Katiba ya nchi, haimruhusu mtu yeyote kumtolea maneno ya dhihaka kiongozi wa nchi. “Halima amekosea sana amepindisha kanuni za nchi kwa kutoa maneno ya uchochezi kwa kusema kuwa ‘ipo siku Rais ataagiza wanawake na wanaume watembee vifua wazi’,” alieleza na kuongeza kuwa kauli hiyo ni ya uchochezi kwa Watanzania, na kuwa kiongozi kama mbunge hapaswi kuchochea vitu ambavyo baadaye vitaleta madhara kwa Taifa.