JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limethibitisha kumshikilia mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji kwa mahojiano baada ya kukutwa na jora 43 za sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na mihuri 39 ya kampuni tofauti tofauti.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lucas Mkondya alisema Manji anashikiliwa na jeshi hilo tangu Julai mosi baada ya kukutwa na vitu hivyo katika ghala lake la Quality Motors, lililopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam.“Ni kweli tunamshikilia tangu Jumamosi tunaendelea kumhoji kwa vitu alivyokutwa navyo ili atuambie alivipataje na anavyo kwa madhumuni gani wakati yeye sio mwanajeshi na amekaa navyo kwake,” alieleza Mkondya.
Akizungumzia endapo Manji atafikishwa mahakamani baada ya mahojiano, Kaimu Kamanda Mkondya alisema baada ya kukamilisha mahojiano na kupata taarifa kamili, wataangalia kama atapelekwa mahakamani kutokana na majibu yake. “Tunasubiri tumalize mahojiano tupate na maelezo yake ili tuone yamekwendaje na kama atafikishwa mahakamani kulingana na mahojiano yatakavyokwenda,” aliongeza Mkondya.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Manji kushikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano. Februari mwaka huu, Manji aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality Group kabla ya kustaafu Julai mwaka jana, alishikiliwa kwa mahojiano baada ya kudaiwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. Katika hatua nyingine, Manji na wenzake wamepeleka maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuomba Jeshi la Polisi kuwaachia huru kwa kuwa wanashikiliwa isivyo halali kwa tuhuma zinazohusiana na sare za JWTZ.
Aidha, wameomba mahakama itoe amri kwa jeshi hilo kuwataka wawapeleke waombaji mahakamani washughulikiwe kwa mujibu wa sheria. Mbali na Manji, waombaji wengine katika kesi hiyo ni Deogratius Kisinda na Thobias Fwere ambao wamewasilisha maombi hayo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO).
Katika hati ya kiapo iliyoungwa mkono na maombi hayo, Wakili wa washitakiwa, Hudson Ndusyepo alidai walalamikaji walikamatwa na kushikiliwa na ZCO kwa nyakati tofauti; Kisinda alikamatwa Juni 30, mwaka huu saa 10 jioni wakati Manji na Fwere walikamatwa Julai mosi saa 5 katika Jengo la Quality Center, Barabara ya Nyerere.
Ndusyepo alidai kuwa tangu siku hiyo mpaka sasa, walalamikaji wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi na kwamba alifahamishwa na ZCO kuwa walikamatwa kwa tuhuma za kutenda kosa linalohusiana na sare zilizokutwa kwenye stoo ya Quality Motors Limited. Pia alidai baada ya kukamatwa kwa walalamikaji hao, aliwaombea dhamana, lakini maombi hayo yalikataliwa kwa sababu zisizojulikana ambapo walikuwa wakifuatilia dhamana za waombaji tangu walipokamatwa.