Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha inaunganisha mikoa yote na umeme ili kuhakikisha viwanda vinavyoanzishwa nchini vinakuwa na uhakika wa nishati hiyo muhimu na kwamba inaendelea vizuri kutokana na miradi kadhaa ya kuzalisha umeme kuendelea kuimarika.

Majaliwa aliyasema hayo jana baada ya kutembelea ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi II na kuelezea kuridhishwa na hatua ya ujenzi huo, huku akitaka wakandarasi na wafanyakazi wa mradi huo kufanya kazi kwa bidii ili uweze kukamilika kwa wakati.
Aidha, amemtaka Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe kuhakikisha anafanya mazungumzo na makatibu wakuu wa wizara nyingine iwapo kutakuwa na vikwazo vyovyote vinavyoweza kuchelewesha mradi huo.
Akizungumza na wafanyakazi wa mradi huo pamoja na wananchi baada ya kukagua mradi huo, Majaliwa alisema, mkakati wa serikali ni kuongeza kiwango cha umeme unaozalishwa katika vyanzo mbalimbali ili kuwawezesha Watanzania kupata umeme.
Alisema sababu ya kuongeza umeme ni ili uweze kufika hadi vijijini kwa wananchi na kwamba mkakati wa kuanzisha Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ni kuhakikisha watu wote vijijini wanapata umeme wa kutosha.
“Tukiwa na mkakati huu tunakwenda sambamba na mkakati wa kukaribisha wawekezaji wanaounga mkono serikali yetu kwenye mkakati wetu wa viwanda, kwamba tunataka tupate umeme wa kutosha ili wawekezaji wa viwanda na wote wanaohitaji umeme wawe na umeme wa kutosha na wa bei nafuu,” alisema Majaliwa.
Alisema ili mwito wa uwekezaji na ujenzi wa viwanda vya ukubwa tofauti nchini uweze kufanikiwa ni lazima kupeleka umeme wa gharama nafuu na wa kutasha ili kila kiwanda kiweze kupanua wigo wa uzalishaji kwa kutumia umeme unaopatikana nchini.
Aliongeza, mkakati wa kuongeza vyanzo vya umeme vya Kinyerezi awamu ya kwanza hadi ya nne na mradi wa Mradi wa Umeme Stiegler’s Gorge ni kuzalisha umeme mwingi ambao utaingizwa katika gridi ya taifa.