|
MWENYEKITI wa Chama cha United Democratic (UDP), John Momose Cheyo maarufu kama `Bwana Mapesa’ amesema jukumu la viongozi wastaafu ni kuwaweka pamoja watanzania na siyo kuwafarakanisha.
Aidha, amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais wa awamu ya tano, John Magufuli na kuijenga Serikali imara, yenye kulinda maslahi ya nchi na ustawi wa watu wake.
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam wakati akitambulisha ofisi za chama hicho zilipohamia Mwananyamala A, Cheyo alisema anashangazwa na mawaziri wakuu wastaafu ambao walihamia upinzani.
“Upinzani sio kupinga kila jambo, wastaafu jukumu lao ni kufanya mambo ya kutuweka pamoja na sio kutufarakanisha,” alisema Cheyo. Alisema kuingiza mambo ya dini katika siasa ni kutafuta mfarakano baina ya wananchi na kwamba kwa maoni yake kiongozi ambaye ameshika nafasi kubwa kama Waziri Mkuu hatarajiwi kuliingiza taifa katika mafarakano.
Cheyo alisema Tanzania imepata Rais ambaye akipata jambo analifanyia kazi mara moja kwa manufaa ya taifa hivyo watu wamuunge mkono bila kujali vyama vyao. “Maendeleo hayana vyama, Rais tuliye naye anafanya mambo na yanaonekana tumuunge mkono tuachane na itikadi za vyama, au wanataka tusubiri mpaka chama fulani kiingie madarakani ndipo tupate maendeleo?” alihoji Cheyo.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa alimtaka Rais Magufuli kuwaachia huru mashehe wa Uamsho wanaoshikiliwa kwa zaidi ya miaka minne sasa.
Aidha, Lowassa amewataka Waislamu kuwa ngangari katika kudai haki kwa mashehe hao akisema wamekuwa baridi sana. Hata hivyo, Rais Magufuli, akiwa katika ziara yake bandarini hivi karibuni, aliwataka wanasiasa kuchunga midomo yao kutetea mashehe waliopo mahabusu, akiwataka kuacha kuzungumza hata wasiyoyajua.
Alionya hayo wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni. “Nataka polisi mfanye kazi zenu … hawa wanaoropokaropoka waisaidie polisi kupeleleza. Msiogope cha sura, mwendo wake awe na speed (kasi) ya kukimbia, ya polepole, atayaeleza vizuri akiwa pale lockup (mahabusu).
“Niwaombe wanasiasa ambao wameshindwa ku-control (kudhibiti) midomo yao…saa nyingine wanazungumza hata mambo wasiyoyajua. “Kuna watu wamekufa zaidi ya 35, askari 15, mtu anatoka pale anazungumza kuwa wamekaa mno. Wajifunze kufunga midomo yao wakati Serikali inafanya kazi yake. Kuna mambo makubwa katika nchi hii tunayoshughulika nayo.
0 Comments