Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliokuwa umefuta kandarasi ya kupiga chapa karatasi za kura za urais kufuatia kesi iliyokuwa imewasilishwa na muungano wa upinzani.
Majaji wa mahakama ya rufaa wamesema mahakama hiyo ya chini ilikosea ilipoamua kwamba wananchi walifaa kushirikishwa katika uamuzi wa kutoa kandarasi hiyo ya thamani ya $24m (£18m) kwa kampuni ya Al Ghurair kutoka Dubai.
Mahakama hiyo imesema si lazima kwa taasisi ya serikali inapoamua kutoa zabuni moja kwa moja kushirikisha wananchi katika kufanya uamuzi au hata kufikia uamuzi wenyewe wa kutumia njia hiyo kutoa kandarasi hiyo.
Aidha, majaji hao wamesema mahakama ilifaa kuzingatia maslahi ya wananchi na haki yao ya kushiriki katika uchaguzi huru na wa haki.
Wamesema ni lazima uchaguzi mkuu ufanyike tarehe 8 Agosti na majaji wa Mahakama Kuu walifaa kuzingatia muda uliopo kwa Tume ya Uchaguzi (IEBC) kujiandaa ili kufanikisha uchaguzi huo.
"Walitumia mamlaka yao vibaya bila kuzingatia ratiba iliyopo," majaji hao walisema kwenye uamuzi wao.
Kila mhusika ametakiwa kugharimia mwenyewe gharama aliyoingia katika rufaa hiyo pamoja na wakati wa kesi iliyokuwa katika Mahakama Kuu.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake tarehe 12 Julai ilikuwa imesimamisha uchapishaji wa karatasi za kura za urais na kuitaka IEBC itoe zabuni upya kwa kuwashirikisha wananchi.
Upigaji chapa wa karatasi za kura za nyadhifa hizo nyingine ulikubaliwa kuendelea.
IEBC Jumanne wiki hii ilipokea sehemu ya kwanza ya karatasi za kura za nyadhifa za ugavana, useneta, ubunge, wawakilishi wa wanawake na wawakilishi wa wadi.
0 Comments