UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI LA MRADI WA KUBORESHA BANDARI YA DSM 02 JULAI 2017

Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli ameawaonya baadhi ya Wanasiasa kuacha
mara moja tabia ya kuwatetea watu wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama kwa
tuhuma za kujihusisha na uhalifu.



Rais Magufuli ametoa
onyo hilo leo Jijini Dar es Salaam wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa
uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam.


“Kuna mwanasiasa anazungumza
kuwa hawa watu wamekaa sana lokapu (mahabusu) waachiwe wakati hawa watu wanahusika
na mambo ya ajabu katika nchi. 


“Kuna watu wamekufa
kule zaidi ya 35, maaskari zaidi ya 15 na wanaohusika ni pamoja na hao lakini
mtu anatoka anazungumza kwamba wamekaa mno. Unaweza ukaona ‘by implication’
kwamba huyu lazima anahusika kwa njia moja au nyingine”, alionya Rais.


Amewataka wanasiasa
wa namna hiyo kujifunza kunyamaza wakati serikali inafanya kazi yake. 


Aidha Rais Magufuli
alieleza kusikitishwa na mmoja wa wanasiasa ambaye kimsingi hajawahi kusimama hata
siku moja kulaani mauaji ya watu wasio na hatia yanayotokea lakini kwa kutaka
sifa za kisiasa alisisimama hadharani kutaka wahalifu waachiwe. 


Alisema hivi karibuni
jeshi la Polisi lilikamata sare 5000 za jeshi na wanaohisiwa kuhusika ni pamoja
na ambao tayari wanashikiliwa na vyombo vya dola lakini bado mtu anaingiza
siasa kwa kuwatetea wahalifu.


Rais Magufuli ambaye
pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini, amelitaka jeshi
la Polisi kumhoji kwa kina mwanasiasa yeyote anayetetea wahalifu kwani anaweza
kuwa nae anahusika.


“Nataka Polisi mfanye
kazi zenu, hawa wanaoropoka waisadie polisi kupeleleza. Msiogope cha sura au
mwendo wa mtu awe na mwendo wa spidi au pole pole atayaeleza vizuri atakapo
kuwa mle lokapu.


Ameeleza kuwa yeye
kama Rais moja ya majukumu yake ni kulinda usalama wa Watanzania na kuusimamia
kwa nguvu zote na kwamba maendeleo yaliyopo yanakuja kwa sababu nchi ni
slalama.


Amewaomba Watanzania wote bila kujali itikadi za
vyama vyao kutanguliza uzalendo na kutetea maslahi ya nchi.