Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi.
WATU sita wanaotuhumiwa kujihusisha na uhalifu katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani wameuawa katika mapambano ya kurushiana risasi na polisi, tukio lililofananishwa na sinema za kivita.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amethibitishwa kuwapo kwa tukio hilo la alfajiri ya kuamkia jana Mtaa wa Fumagila Mashariki, Kata ya Igoma wilayani Nyamagana Alisema kati ya waliouawa, mmoja tu, Selemani Juma ndiye aliyefahamika na wengine watano hawajafahamika majina yao.

Alisema majambazi hao walipatikana na silaha aina ya AK 47 yenye namba za usajili 1971E3445 na magazini zake mbili zikiwa na risasi 30 kila moja, silaha nyingine nne zilizotengenezwa kienyeji, na risasi zingine 36 za AK 47 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye begi na sare za jeshi na mikanda yake zinazodaiwa kutumiwa na majeshi ya nchi jirani.
Vitu vingine vilivyokamatwa kwa mujibu wa Kamanda Msangi ni kofia sita za kuficha uso na mabegi matatu yaliyokuwa yamehifadhi risasi, pikipiki moja yenye namba za usajili T 815 DAA aina ya Sanya na baiskeli mbili.
Alisema, awali polisi walipokea taarifa kutoka kwa wasiri kwamba baadhi ya wahalifu wanaofanya shughuli za uhalifu katika wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani wamekimbilia mkoani Mwanza na kujificha katika eneo la Fumagila.
“Polisi walifanya ufuatiliaji wa haraka wa taarifa hizo katika sehemu mbalimbali za jiji, mkoa wa Mwanza na maeneo jirani na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye alikiri kufanya uhalifu na kuwapa polisi ushirikiano kwa kuwapeleka hadi eneo la Fumagila ambapo alidai wenzake walikuwa wamejificha”, alifafanua.
Alisema baada ya polisi kufika katika eneo la Fumagila, ghafla majambazi hao walikurupuka na kuanza kuwarushia polisi risasi, lakini kutokana na umahiri wa askari polisi walijibu mashambulizi na kufanikiwa kuwaua sita huku wawili wakifanikiwa kutoroka kutoka kwenye eneo la tukio.
“Polisi inawasaka majambazi hao waliotoroka na hakuna askari polisi aliyejeruhiwa kwa risasi au kupoteza maisha kwenye tukio hilo”, alisema na kuongeza miili ya watu hao imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando.
Aidha alisema kuwa zimepatikana taarifa kuwa majambazi waliouawa ndio walioshiriki katika unyang’anyi wa kutumia silaha Juni 15 mwaka huu katika Kiwanda cha mikate cha Victoria, jijini hapa na kupora Sh milioni 30, kisha kukimbilia kusikojulikana, ambapo kesi na NY/4747/2017 ilifunguliwa kwa ajili ya tukio hilo.
Katika mtaa huo, Desemba mwaka jana walikamatwa watoto 11 wenye umri wa kati ya miaka sita na 14 baada ya kuizingira nyumba moja kwa lengo la kuwakamata majambazi. Hata hivyo, katika kupurukushani hizo, mmoja wa watu waliokutwa katika nyumba hiyo, alikimbia baada ya kuwarushia askari polisi bomu la mkono.
Aidha, katika tukio hilo watu watatu waliosadikiwa kuwa ni majambazi waliuawa, huku polisi wakikamata bunduki mbili aina ya SMG na AK 47, magazini saba, bastola moja na risasi 183. Hata hivyo, wananchi wakazi wa eneo hili waliiteketeza kwa moto nyumba husika mara baada ya askari kuondoka na watuhumiwa.
Mwingine afa Kibiti Katika tukio jingine, mkazi wa Kitongoji cha Nyambwanda katika jijini cha Hanga wilayani Kibiti, Hamisi Ndikanye (54) ameuawa na watu wasiojulikana baada ya kupigwa risasi mbili usiku akiwa nyumbani kwake.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu aliyejitambulisha kuwa ni Hamisi Saidi, takribani watu watano walifika nyumbani kwa marehemu majira ya saa sita usiku na kumpiga risasi mbili Hamisi, baada ya kumfunga kitambaa usoni mkewe.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kibiti, Onesmo Lyanga, akizungumzia tukio hilo alisema askari wake wamekwenda eneo la tukio kwa uchunguzi zaidi. Mganga wa Kituo cha Afya Kibiti, Sadock Bandiko alithibitisha kifo hicho, akisema amepigwa risasi mbili, moja kichwani na nyingine mgongoni.