Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) akisikiliza maelezo kutoka kwa mama Abia Magembe kuhusu bidhaa zinazotokana na zao la muhogo. Kushoto kabisa ni Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cebada na kulia ni Mratibu wa mradi huo nchini Tanzania, Secelela Balisidya.


NAIBU Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Selemani Jaffo, amesema halmashauri zinawajibu wa kuunga mkono
jitihada za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.


Kutokana na hali hiyo, ameonya mtu yeyote asikwamishe
jitihada zinazofanywa na akinamama washiriki wa mradi wa Green Voices Tanzania
huku akiahidi kuwa serikali iko nao bega kwa bega.
Alisema kwamba, endapo kuna mtu katika idara zilizo chini ya
wizara yake atakwamisha jitihada zao, basi akinamama hao wawasiliane naye moja
kwa moja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa
Green Voices nchini Tanzania uliofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini
Dar es Salaam, Naibu Waziri Jaffo alisema kwamba, wizara yake ndiyo yenye
jukumu kubwa la kuwawekea mazingira mazuri akinamama hao kutekeleza miradi yao
chini ya halmashauri husika, hivyo akawaahidi kuwapatia ushirikiano wa kutosha
kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na suala la mazingira linapewa
kipaumbele.
Mradi wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa ya Dar es
Salaam, Pwani, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro, kukiwa na miradi 10
ikiwemo ya kilimo cha mihogo, kilimo cha matunda, uyoga, ufugaji wa nyuki,
ukaushaji wa mbogamboga na utengenezaji wa majiko rafiki wa mazingira.
Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia Cedaba (kushoto) akiwa na Leocadia Vedasto kutoka Ukerewe anayeratibu kilimo cha viazi lishe pamoja na usindikaji wa bidhaa zake. Katikati ni mdau mwingine aliyehudhuria uzinduzi wa awamu ya pili ya Mradi wa Green Voices Tanzania.
Bidhaa za mbogamboga zilizokaushwa kutoka Morogoro.
 Akinamama walioanzisha miradi hiyo – miradi na mikoa
watokayo vikiwa kwenye mabano –ni Regina Kamuli (Mkuranga, Pwani –
Majiko
Banifu
), Abiah Magembe (Kisarawe, Pwani – Usindikaji
wa Muhogo na Mtama
), Magdalena Bukuku (Kinondoni, Dar es Salaam – Kilimo
cha Uyoga
), Mariam Bigambo (Dakawa, Morogoro – Ufugaji
wa Nyuki
), na Esther Muffui (Morogoro – Ukaushaji
wa Mboga na Matunda
).


Wengine ni Farida Makame (Kilimanjaro – Majiko
ya Umeme-Jua
), Leocadia Vedastus (Ukerewe, Mwanza – Kilimo
na Usindikaji wa Viazi Lishe
), Monica Kagya (Kisarawe, Pwani – Ufugaji
wa Nyuki
), Dkt. Sophia Mlote (Kinyerezi, Dar es Salaam – Kilimo
Hai cha Nyanya na Mbogamboga
), na Evelyn Kahembe (Uvinza, Kigoma – Kilimo
cha Matunda).
Kupitia miradi hiyo, zaidi ya wanawake 300 wamepatiwa
mafunzo mbalimbali huku program nyingine za mafunzo kwa vitendo zikiendelea
katika makundi yao.
 “Serikali ya Tanzania
na hasa wizara hii, na wizara hii Mheshimiwa Rais mwenyewe ni wizara yake,
naomba niwahakikishie kwamba tutashirikiana na Green Voices kwa nguvu zote na nitawapa
pasiwedi ya kuwasiliana na ofisi yangu moja kwa moja ili kama mnakwama mambo
yenu yaweze kwenda huko katika halmashauri mlipo,” alisema Jaffo, ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani.
Akaongeza: “Nitawaunganisha na mkurugenzi maalum wa idara za
serikali katika wizara yangu, kwamba ninyi mkikwama katika halmashauri kwa jambo
lolote lile mnawasiliana naye  moja kwa
moja mradi mambo yenu yaweze kwenda mpate sapoti, sauti ya wanawake iweze
kusikika, mambo ya mazingira yaweze kubadilika, kilimo, mifugo na kadhalika ili
mwisho wa siku watu waseme kwamba kuna kundi la watu walikwenda Hispania na
wakajifunza wakaleta mabadiliko nchini.”
Aidha, Naibu Waziri Jaffo alisema kundi hilo la akinamama wa
Green Voices ni muhimu na serikali itahakikisha inawaunga mkono kwa kila hali.
"Ninyi ni kioo cha jamii na watu wengi wanatakiwa
wajifunze kutoka kwenu. Kumbukeni, katika suala la mazingira maeneo mengi
yameathirika sana, mnaweza kuona jinsi maeneo mengi yanavyokumbwa na mafuriko
kutokana na watu kukata miti na kuharibu mazingira, wakati mwingine
tunashuhudia ukame wa kutisha.
“Kwahiyo ninyi mradi wenu unakwenda kukabiliana na
changamoto hizi, ni muhimu sana, mna wajibu mkubwa sana kwa sababu suala la
mazingira ni muhimu na linaathiri dunia.
“Tunatakiwa tutoke katika miradi isiyo halisi (artificial projects) na kwenda kwenye miradi
halisi ili tuweze kubadilisha maisha ya watu.”
Vile vile, aliwaasa akinamama hao kwamba, wakienda huko waongee
lugha rahisi na wananchi ili iwe rahisi kueleweka.
“Ninyi hapa wote ni wasomi, lakini mkienda huko ongeeni
lugha rahisi ili mwananchi wakawaida akisikia aweze kuielewa na kuleta
mabadiliko ya kweli. Mama mwingine hajasoma hata darasa moja na inawezekana
kuwepo kwako wewe kukabadili maisha yake,” alisema.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jaffo, akizungumza katika uzinduzi huo.  
Secelela Balisidya akipokea cheti.
Mmoja wa washiriki wa mradi wa Green Voices, Mariam Bigambo,
mkulima wa Mvomero ambaye amejikita katika ufugaji wa nyuki akiwa na kikundi
cha wanawake 15, alisema kwamba licha ya umuhimu wa mradi huo, lakini
wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinakwamisha maendeleo yao.
“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni kushushwa kwa
mizinga yetu na watu wasiojulikana kwa sababu tumeiweka porini,” alisema na
kuongeza: “Kila mara tunakuta mizinga yetu imeshushwa, tumekwishatoa taarifa
kwa serikali ya kijiji pamoja na kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mvomero na hata Polisi.”
Aidha, alisema kwamba, ufugaji wa nyuki unahitaji uvumilivu
na mpaka sasa baadhi ya wanakikundi wamevunjika moyo kwa sababu bado
hawajanufaika na matunda ya kazi yao.
Kutokana na hali hiyo, alisema, wameamua pia kugeukia kilimo
cha uyoga ili kuongeza tija.
Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela
Balisidya, alisema awamu ya kwanza ya mradi huo ililenga katika uanzishwaji na
uzalishaji, lakini awamu ya pili inalenga kuwapatia stadi akinamama ili
kuboresha bidhaa wanazozizalisha ili ziongezeke ubora la kuwaletea tija.
“Hivi sasa katika awamu ya pili akinamama watapatiwa mafunzo
ya namna ya kutengeneza bidhaa zao kama vifungashio ili kuongeza ubora na
thamani na tunataka bidhaa zao ziingie sokoni katika viwango ambavyo
vinakubalika,” alisisitiza.
Akizungumza katika uzinduzi huo wa awamu ya pili, Mratibu wa
mradi wa Green Voices kutoka Hispania kutoka taasisi ya Women for Africa
Foundation inayodhamini mradi huo, Alicia Cebada, alisema
wamefarijika na mradi huo kwa kuwa umeonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania

katika awamu ya kwanza na ndiyo maana wameamua kuwaongezea uwezo akinamama hao
katika awamu hii.
 “Tumekuwa
tukiwasiliana mara kwa mara na Secelela (Mratibu wa Green Voices Tanzania)
kuhusu mafanikio na changamoto za mradi huu na kwa kweli tunafarijika kuona
miradi yote inakwenda vizuri,” alisema Alicia.
Alisema, changamoto pekee ambayo ipo mbele yao ni
kuhakikisha miradi hiyo inasimama na kuwafundisha wanawake wengi kadiri wawezavyo
ili kuhakikisha wanajiletea maendeleo katika maeneo yao kiuchumi na kijamii.
Mwaka 2016 rais wa mfuko wa Women for Africa Foundation,
Mama Maria Tereza Fernandez de la Vega, alizuru nchini Tanzania na kushiriki
uzinduzi wa mradi huo Julai 11, 2016 ambapo ulizinduliwa rasmi na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.
Katika uzinduzi huo, Mama Samia aliahidi kwamba serikali
yake itahakikisha inakuwa bega kwa bega kusaidia miradi hiyo iwe endelevu ili
kuunga mkono juhudi za utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya
tabianchi, kuongeza uhakika wa chakula, kuwakwamua wananchi na umaskini pamoja
na kuongeza ajira, hasa kwa wanawake.
Kwa upande wake, Mama Maria Tereza, ambaye ni makamu wa rais
mstaafu wa Hispania, alieleza kufurahishwa kwake na jitihada za akinamama wa
Tanzania na kusema taasisi yake inaangalia namna ya kuwasaidia zaidi.