Waziri wa usalama nchini Kenya Jenerali Mstaafu Joseph Nkaissery amefariki dunia.
Waziri huyo amefariki dunia saa chache baada yake kulazwa katika hospitali ya kibinafsi ya Karen kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Taarifa za kifo chake zimetangazwa na mkuu wa utumishi wa umma Bw Joseph Kinyua mwendo wa saa kumi na moja alfajiri.
"Ni kwa huzuni kubwa na mshangao kwamba tunatangaza kifo cha ghafla cha Waziri wa Usalama wa Ndani Jenerali Mstaafu Joseph Nkaissery," taarifa ya Bw Kinyua imesema.
"Taifa litaendelea kupashwa habari zaidi punde maelezo yatakapopatikana."
Jenerali Joseph Kasaine ole Nkaissery, 67, amefariki siku chache baada ya mwanasiasa mkongwe G.G. Kariuki aliyekuwa seneta wa jimbo la Laikipia kufariki dunia.
Waziri huyo alizaliwa mwaka 1949 na alihudumu katika jeshi kwa miaka 29 kabla ya kuingia katika siasa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2002 ambapo alimshinda David Sakori wa chama cha KANU wakati wa kustaafu kwa Rais Daniel arap Moi katika eneo bunge la Kajiado ya Kati.
Mwaka 2007, alichaguliwa tena kuwa mbunge wa eneo hilo kwa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) chake Raila Odinga na wakati wa kuundwa kwa Serikali ya Muungano wa Kitaifa kati ya Bw Odinga na Rais Mwai Kibaki, alipewa wadhifa wa Waziri Msaidizi wa Ulinzi.
Ni wakati wake ambapo Kenya iliingia nchini Somalia, baada ya makubaliano na serikali ya taifa ya Somalia, kupambana na wanamgambo wa al-Shabab mwaka 2011 chini ya Operesheni Linda Nchi.
Alichaguliwa tena kuwa mbunge uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 kupitia ODM lakini Desemba mwaka 2014, baada ya kufutwa kazi kwa aliyekuwa waziri wakati huo Joseph Lenku kutokana na kuongezeka kwa mashambulio ya kigaidi ya al-Shabab, aliteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Ndani, Usalama na Uratibu wa Serikali ya Taifa na Rais Uhuru Kenyatta.
Hatua hiyo iliughadhabisha upinzani ambao ulitazama hatua hiyo kama mpango wa kuudhoofisha upinzani.
Jenerali Nkaissery alijiuzulu wadhifa wake wa ubunge na akaapishwa kuwa waziri 24 Desemba, 2014.
Akiwa waziri, Kenya ilionekana kufanikiwa kuwadhibiti al-Shabaab na mashambulio ndani ya nchi yakapungua.
Alikuwa miongoni mwa mawaziri walioitetea sana serikali na uchaguzi ulipokaribia, alikuwa akipuuzilia mbali vitisho vya upinzani na kuonya kwamba hatawavumilia watu wanaotaka kuvuruga amani nchini Kenya.
Amekuwa waziri wa pili wa usalama kufariki duniakatika kipindi cha miaka mitano. Juni mwaka 2012, waziri usalama wa wakakti huo Prof George Saitoti, ambaye alikuwa wakati mmoja amehudumu kama makamu wa rais chini ya Rais Moi, alifariki dunia kwenye ajali ya ndege eneo la Ngong viungani mwa mji wa Nairobi.
Alifariki dunia pamoja na waziri wake msaidizi Joshua Orwa Ojode.