Waziri
wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe Dkt Dk Charles Tizeba akisisitiza jambo kabla ya
kufungwa kwa Maonesho ya Nanenane katika viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi  tarehe 8 Agosti 2017.



Na Mathias Canal, Lindi

Serikali imetangaza dhamira ya
kuhakikisha kuwa inaboresha zaidi Sekta ya Uvuvi ili kuongeza uzalishaji na
tija, ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi Mheshimiwa Dkt Charles Tizeba  amesema hayo wakati wa kumkaribisha
mgeni rasmi Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan katika kilele cha
maadhimisho ya sikukuu ya wakulima, nane nane kitaifa, katika viwanja vya
Ngongo katika manispaa ya lindi jana tarehe 8/8/2017.

Alisema kuwa kwa kufanya hivyo
serikali itahamasisha watu wengi kufuga samaki katika mabwawa na vizimba ili
waweze kuzalisha samaki wengi zaidi sambamba na kuboresha zaidi uvuvi wenye
tija na ambao ni endelevu. 

Dkt Tizeba amemshukuru  Mhe.
Makamu wa Rais kwa hatua zizochukuliwa  na Ofisi yake za kulinda mazingira
ya nchi, ikiwa ni pamoja na kurahisisha upatikanaji wa cheti cha kukidhi
matakwa ya utunzaji mazingira.

Alisema ipo Mipango
mbalimbali iliyowekwa na wizara, hivyo itatekelezwa kwa ufanisi zaidi kwa
kuhimiza ushiriki wa Sekta Binafsi, kuwekeza zaidi katika Kilimo, Mifugo na
Uvuvi kwa kuzingatia mnyororo wa thamani ili kutekeleza azma ya Serikali ya
Awamu ya Tano ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo au kabla ya mwaka 2025. 

Alisema jambo hilo linaendelea
vyema kwa kuhuisha kauli mbiu ya Maonesho ya Nanenane kwa mwaka 2017 isemayo; Zalisha kwa Tija
Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia uchumi wa kati

Dkt Tizeba aliongeza kuwa
Kupitia Kaulimbiu hiyo wizara yake inahimiza, matumizi ya nyenzo sahihi kama
matrekta, na mashine nyingine za uzalishaji na usindikaji, kuongeza uwekezaji
katika viwanda vodogo,  vya kati na vikubwa,  sambamba na kuweka
mazingira bora yanayovutia Sekta Binafsi kuwekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi
kupitia mnyororo wa thamani.

Aidha, alisema kuwa katika
Maadhimisho hayo, Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine
walipata nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na hatimaye Sekta ya
kilimo iweze kuongeza uzalishaji na tija zaidi. 
Aliongeza kuwa uzalishaji,
wizara itajihakikishia ziada kubwa ya chakula na malighafi za kutosha katika
viwanda vilivyopo na vinavyotarajia kuanzishwa. Kama ambavyo, inafahamika kuwa
upatikanaji wa masoko ya uhakika, utachochea zaidi uzalishaji wa mazao ya
kilimo, mifugo na uvuvi, uhakika wa bei kwa mazao na bidhaa zinazozalishwa na
Mkulima, Mfugaji na Mvuvi atakayewekeza zaidi katika uzalishaji.

MWISHO