Na Jumia Travel Tanzania

Miongoni mwa matukio yanayosisimua zaidi kwenye mchezo wa soka ni mipambano ya watani wa jadi. Katika nchi nyingi barani Afrika ukiwauliza kwa harakaharaka mashabiki wengi wa soka ni mechi zipi huwa wanazisubiria sana utawasikia wanakutajia michezo kama vile Real Madrid na Barcelona, Manchester United na Manchester City, Inter Milan na AC Milan, Liverpool na Manchester United, Chelsea na Arsenal au Bayern Munich na Borussia Dortmund.
Kutokana na umaarufu wa soka la nchi za Ulaya imekuwa ni rahisi kwa mechi zao kufuatiliwa kwa urahisi ukilinganisha na huku Afrika. Lakini hiyo haimaanishi kwamba bara la Afrika nalo halina michezo ya namna hiyo ambayo ikiwa inakaribia homa miongoni mwa mashabiki huwa juu kuliko kawaida.

Ukweli ni kwamba mechi za namna ya mifano iliyotajwa hapo juu zipo na zimekuwa zikichezwa kwa miaka mingi tu.kw au pengine inawezekana ukawa unazisikia tu lakini haujui umuhimu uliopo pindi zinapokutana. Jumia Travel imekukusanyia orodha ya mechi kali za mpira wa miguu ambazo timu zikikutana kunakuwa ni patashika, presha na vimbwanga vya kila aina.  
Orlando Pirates dhidi ya Kaizer Chiefs (Afrika ya Kusini) -  Soweto derby. Kama yalivyo mapambano mengine ya watani wa jadi, mchezo huu ni zaidi ya mpira wa miguu kwani ni uhasama hasa. Mchezo ambao umpewa jina la ‘Soweto derby’ huzikutanisha timu za Orlando Pirates na Kaizer Chiefs mara kadhaa ndani ya mwaka katika jiji la Johannesburg. Uhasama wa timu hizi mbili unakuja kutokana na kuwa zote zinatokea sehemu moja. Kaizer Chiefs ilianzishwa na aliyekuwa mmojawapo wa wachezaji wa Orlando Pirates, Kaizer Motaung.
   
Wydad Casablanca dhidi ya Raja Casablanca (Morocco) - Casablanca derby. Hakuna ubishi kwamba nchi za Afrika ya Kaskazini zimebarikiwa kuwa na vipaji lukuki vya mpira wa miguu ambapo mpaka hivi sasa vinaliwakilisha vema bara hili sehemu mbalimbali duniani. Katika mji wa Casablanca kwenye nyakati tofauti za mwaka kunakuwa na mchezo mkali ambao huzikutanisha timu za Wydad Casablanca na Raja Casablanca ambao pia hujulikana kama ‘Casablanca derby’. Mchezo wa watani wa jadi hawa mara nyingi hupigwa katika uwanja wa Mohammed V Stadium ambapo licha ya kuonyesha nani ni fundi wa kusakata kandanda lakini pia ni juu ya nani ni bora katika anga za kuliwakilisha jiji na nchi kwa ujumla.  
Al Ahly dhidi ya Zamalek (Misri) - Cairo derby. Linapokuja suala la mchezo wa soka basi mashabiki wa timu za Al Ahly dhidi ya Zamalek ni nambari moja kwa kuzishangilia timu zao. Mojawapo ya mitanange mikali kabisa ya soka ambayo hutawaliwa na presha na msisimko mkubwa ni pindi timu hizi zinapokutana ambao pia umepewa jina la ‘Cairo derby.’ Inapofikia siku ya mechi hii hali ya hewa ya jiji zima la Cairo hubadilika kutokana na homa ya mchezo huo. Mbali na kuwa ushindani huwa ni wa kisoka lakini kwa upande mwingine ni wa kisiasa zaidi.
    
Club Africain dhidi ya Espérance Sportive de Tunis (Tunisia) - Tunis derby. Katika jiji la Tunis kwenye ratiba tofauti za mchezo wa soka huzikutanisha timu mbili zinazowakilisha jiji hilo za Club Africain na Espérance Sportive de Tunis. Ushindani mkubwa katika mchezo huu umekuwa na historia tofauti ambapo hapo awali ulihusishwa na matabaka kama vile ilisemekana timu ya Espérance ilikuwa ikimilikiwa na serikali na tabaka la juu la watu wa mji wa Tunisia huku Club Africain ikimilikiwa na watu maarufu wa matabaka tofauti. Lakini hiyo imebadilika na ikawezekana kutokuwa na ukweli ndani yake kwani unaweza kukuta watu wa familia moja wanashabikia hizo kwa wakati mmoja.
  
Simba S.C. dhidi ya Young Africans S.C. (Tanzania) - Dar es Salaam au Kariakoo derby. Tukiachana na umaarufu wa mchezo wa mpira wa miguu katika nchi za Afrika ya Kuskazini pia katika kalenda za soka barani Afrika huwa inapigwa mechi kali sana kwenye ukanda wa Afrika ya Mashariki baina ya timu za Simba na Young Africans au Yanga ambazo zote hutokea jiji la Dar es Salaam. Mbali na timu hizo kukutana katika michezo kadhaa ya ligi kuu pia kuna michezo mingine ni pamoja na ngao ya jamii, kombe la shirikisho la mpira wa miguu, kombe la mapinduzi ne mingineyo. 
Kama ni mgeni kwenye jiji la Dar es Salaam basi ikifika siku ya mchezo huo utajua homa ya watani wa jadi wa timu hizo mtaani kwani utawatambua mashabiki wa timu hizo kwa mbwembwe, tambo na shamrashamra kwa kuvalia jezi za rangi nyekundu na nyeupe (Simba) huku Yanga ni (kijani na njano). 

Uhasama wa timu hizo ambazo zinatokea katika eneo moja la Kariakoo si tu kuhusu mpira bali ni heshima juu ya nani ni mfalme na bingwa wa kusakata kandanda nchini Tanzania na kuliwakilisha taifa kwenye anga za kimataifa. Mchezo baina ya timu hizi mbili huwa unapigwa kwenye uwanja wa taifa ambao unao uwezo wa kukusanya mashabiki takribani 60,000.
USM Alger dhidi ya MC Alger (Aljeria). Mchezo huu wa watani wa jadi kama ilivyo mingine huzitenganisha familia na majirani na wakati mwingine huisha kwa ugomvi na vurugu baina ya mashabiki wa pande mbili. Uhasama baina timu ya hizi mbili unahusishwa kwa kiasi kikubwa na historia ya nchi hiyo wakati wa harakati za kudai uhuru. Katika sehemu mbalimbali za nchi ya Aljeria mchezo baina ya timu hizi mbili hubakia kuwa ni tukio la kitaifa kutokana na kuzungumziwa na kupewa nafasi kubwa kwenye vyomo tofauti vya habari.

TP Mazembe dhidi ya FC Lupopo (R.D Congo). Jina la TP Mazembe sio geni miongoni mwa mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania kutokana na wachezaji wa hapa nyumbani Mbwana Samata ambaye alifanikiwa kujitwalia taji la mchezo bora wa ndani wa Afrika na Thomas Ulimwengu kuchezea pale. Katika jiji la Lubumbushi kila mwaka kunakuwa na tukio kubwa la mchezo wa soka ambalo huwakutanisha watani wa jadi kati ya TP Mazembe na FC Lupopo.

Gor Mahia dhidi ya AFC Leopards (Kenya) - Nairobi au Mashemeji derby. Shamrashamra na tambo za mashabiki wa mchezo wa mpira miguu katika mitaa mbalimbali ya jiji la Nairobi huonekana wazi pindi timu za Gor Mahia na AFC Leopards zinapokutana. Mchezo huu ambao una historia ya muda mrefu kwenye soka nchini Kenya huchukuliwa kama ni siku kubwa ambapo mashabiki licha ya kuonyesha uhasama mkubwa lakini ni sherehe, likizo na huchukuliwa kama siku maalum.
Asec Mimosas dhidi ya Africa Sport Abidjan (Ivory Coast) - Abidjan derby. Miongoni mwa tukio baya kutokea pindi timu hizi mahasimu zinazotokea katika jiji la Abidjan nchini Ivory Coast ni mwaka 2001 ambapo vurugu zilitokea ambapo mtu mmoja alifariki huku 30 wakijeruhiwa. Timu ya Asec Mimosas inajivunia kwa kutoa vipaji vikubwa kabisa vya soka nchini humo na duniani wakiwemo Kolo Toure, Didier Drogba na Gervinho.

Al-Merreikh dhidi ya Al-Hilal (Sudani). Uhasama wa timu hizi mbili zinazotokea kwenye jiji la Omdurman nchini Sudan ambapo mnamo mwaka 1934 timu ya Al-Merreikh iliifunga Al-Hilal kwa mabao 2 bila ya majibu ambapo kulikuwa hakuna uwanja enzi hizo. Uhasama baina ya timu hizo mbili pia huchochewa kwa kiasi kikubwa na idadi ya wachezaji kila timu iliyo nayo kwenye kikosi cha timu ya taifa.      
Ipo michezo mingine mingi tu ya watani wa jadi kwenye soka lakini hiyo ndiyo mikubwa ambayo inasubiriwa na kuangaliwa zaidi. Jumia Travel inaamini kwamba sasa utakuwa umeijua na utaanza kuifuatilia kwani kuna burudani nyingi ulikuwa ukiikosa kwa kutoifuatilia. Mechi hizo kutokupewa nafasi kubwa na vyombo vya habari tofauti barani Afrika kama ilivyo kwa ile ya Ulaya haimaanishi kwamba haina ushindani mkubwa.