Bondia Floyd Mayweather amesema kwamba hataonekana tena katika ulingo wa ndondi baada ya kumshinda Conor McGregor katika pigano lililomalizika kwa njia ya knockout katika raundi ya 10.
Hatahivyo Mayweather amesema kuwa iwapo atapata fursa ya kujipatia $300m katika dakika 36 atarudi.

''Mimi sio mjinga, iwapo kutakuwa na fursa ya kutengeza dola $ 300m katika dakika 36 nitarudi kupigana''.
Mayweather ambaye alistaafu baada ya kumshinda Andre Berto mnamo mwezi Septemba 2015 amesema kuwa hakuna kilichosalia kudhihirishia ulimwengu.
Aliongezea Kuwa: Hili ni pigano langu la mwisho hamutaniona tena.Mtu yeyote anayetaka kupigana nami asahau.Najiandaa kuwa mkufunzi wa ndondi ili kuwasaidia mabondia.
Mayweather alikiri kwamba pigano dhidi ya McGregor lilimchukua muda mrefu kumsimamisha mpinzani wake zaidi ya walivyodhania yeye na babake.
''Nilifanya kile ninachoweza kufanya'', alisema. ''Nilipata njia ya kumnasa na kufanikiwa kumpiga.Babangu alidhani kwamba nitamsimamisha katika raundi ya saba ama hata sita''.
''ilituchukua muda mrefu lakini hatimaye tulifanikiwa kufanya kile tunachoweza kufanya''.
Wakati wa pigano hilo Mayweather alionekana kukasirishwa na hatua ya McGregor kumpiga kisogoni.
''Nilimwachia refa kufanya kazi yake,alisema.Siko hapa kumshutumu refa lakini muliona kilichokuwa kikiendelea''.