Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amewapandisha vyeo askari 24 wakati wa ziara yake ya siku moja ya kikazi mkoani Tanga.
Katika askari hao waliopandishwa vyeo, watatu wamekuwa Wakaguzi, wengine watatu watakuwa Sajini Taji, wanane wamepanda na kuwa Sajini pamoja na 10 kuwa Koplo. Akizungumza alipotembelea Ofisi ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Tanga (TPC) ili kuzungumza na wanahabari, IGP Sirro alisema katika lengo la ziara yake hiyo ni kuangalia utendaji kazi na hali ya mazingira wanayofanyia kazi ikiwemo changamoto zinazowakabili ili kuwezesha kufanya maboresho.

“Hii ni ziara yangu ya kawaida kama nilizofanya kwenye mikoa mingine na lengo ni kuwakumbusha wajibu wao ili waweze kutenda haki na kuwa na utayari katika kulinda raia na mali zao pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria kwenye jamii ya hapa Tanga,” alieleza IGP Sirro. Akizungumzia watu wanaofanya matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mkoani Pwani, Kamanda Sirro alisema pamoja na amani kurejea kwenye eneo la Kibiti, lakini kuna haja kwa jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kupata taarifa zao kabla hawajatekeleza uhalifu katika jamii.
“Napenda kuendelea kuwathibitishia Watanzania kwamba Kibiti, Tanga na maeneo yote yako shwari na utulivu nitoe ombi kwa wananchi kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama kuanzia ngazi za vijiji kujaribu kufuatilia ili kuwabaini wahalifu hao kwa sababu wamekuwa wakitawanyika katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini,” alieleza.
Akizungumzia ulinzi katika miundombinu ya bomba la mafuta ghafi, IGP Sirro alisema pamoja na jeshi hilo kushirikiana na mamlaka nyingine za ulinzi na usalama, upo mkakati maalumu wa Polisi unaolenga kuongeza idadi ya askari pamoja na vitendea kazi vya kutosha katika maeneo yote ya mradi ili kuhakikisha unakuwa salama.
Akijibu swali la mmoja wa waandishi kuhusu jeshi hilo kukamata baadhi ya wanasiasa nchini, IGP Sirro alisema, “Polisi tunakamata mtu yeyote tunayeamini kwamba amefanya kosa la jinai na siyo wanasiasa kama baadhi ya wananchi wanavyodhani tunachofanya ni kuwahoji ili kuweza kuwapeleka mahakamani lakini kama mtu hahusiki basi tunamwachia huru.”
Hata hivyo, IGP amepongeza kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari katika kulinda na kuimarisha amani na utulivu na kuwahimiza waandishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya sheria. “Ndugu zangu nchi hii ni ya kwetu nawaomba tuendelee kutanguliza uzalendo mbele ili tusirudishe nyuma maendeleo na ustawi wa nchi yetu,” alieleza.
Katika hatua nyingine, mkazi wa hapa aliyejitambulisha mbele ya waandishi wa habari kwa jina moja la Nuni, aliyekuwa jambazi sugu kati ya miaka ya 1984 hadi 2009 mkoani Tanga maarufu kama ‘Sirro Mdogo,’ alijitokeza na kumshukuru IGP kwa namna alivyomsaidia kuachana na vitendo hivyo wakati alipokuwa Kamanda wa Polisi mkoani humo.
Akizungumza kwa furaha, Nuni alisema anamshukuru IGP Sirro kwa namna alivyomsaidia kwa kumpatia ushauri pamoja na mtaji uliomwezesha kuanzisha biashara ya kuuza nguo za mtumba katika soko la Mgandini lililopo jijini Tanga kwa miaka minane sasa.
“Kwa kweli nimekuja hapa ili kumshukuru huyu mzee kwa namna alivyosaidia kuniokoa kutoka kwenye tabia ya kufanya matukio ya uhalifu hasa ujambazi uliotikisa Mkoa wa Tanga kwa takriban miaka 25 iliyopita hadi nimekuwa raia mwema, nawashauri vijana wengine wajisalimishe polisi ili waweze kusaidiwa kuachana na vitendo vya uhalifu,” alisema Nuni.