|
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa ambaye jana aliteuliwa kuwa Kamanda wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, amesema yuko tayari kuitumikia nafasi hiyo, akisema uteuzi huo ni bahati kubwa kwake.
Akizungumza jana katika mahojiano na gazeti hili, Kamanda Mambosasa alisema amepokea uteuzi huo kwa mikono miwili kwani wengi walitamani kuteuliwa kwenye nafasi hiyo. “Nimepokea uteuzi huo na nimashukuru Mwenyezi Mungu, nawashukuru viongozi wangu walioniona nafaa,” alieleza Kamanda Mambosasa. Alisema sasa yuko tayari kutumikia Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, na anaondoka Dodoma akiwa ameiacha vizuri ikiwa yenye amani na usalama.
“Dodoma naiacha vizuri lakini nitawamisi,” alieleza Kamanda Mambosasa. Kabla ya kuwa RPC Dodoma, Kamanda Mambosasa alikuwa Simiyu kwa wadhifa kama huo. Mapema jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro alimteua kuongoza Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, akichukua nafasi iliyokuwa wazi baada ya uteuzi wake (Sirro) kuwa IGP, Februari mwaka huu.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Barnabas Mwakalukwa, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Gilles Mroto anakuwa Kamanda wa Polisi Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Emmanuel Lukula atarithi nafasi yake Mkoa wa Kipolisi Temeke. Kabla ya uteuzi huo, ACP Lukula alikuwa Ofisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Mbeya.
Mwakalukwa alieleza kuwa aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, na aliyekuwa Kamanda wa mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Neema Mwanga anarejea Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam. Aidha, IGP Sirro amemteua Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Juma Yusuf Ally kuwa Kaimu Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Uteuzi huo unatokana na kustaafu kwa aliyekuwa kamishna wa Polisi Zanzibar, Kamishna Hamdani Omari Makame kwa mujibu wa sheria baada ya kutimiza umri wa miaka 60. Kabla ya uteuzi huo, DCP Juma alikuwa Mkuu wa Utawala na Fedha Makao Makuu ya Polisi Zanzibar. Aidha, jeshi hilo limetoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kufichua taarifa za uhalifu na wahalifu ili tuendelee kuiweka nchi katika usalama.
0 Comments