Rais John Magufuli akiakata utepe kufungua rasmi Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro eneo La Maweni Jijini Tanga
RAIS John Magufuli amesema anamshangaa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kwa kuchelea kuwanyang'anya umiliki baadhi ya wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda vilivyobinafsishwa na serikali miaka 20 iliyopita na kusababisha matumizi ya maeneo hayo kuhujumiwa.
Amemtaka waziri huyo kutoangalia sura au maamuzi yaliyopitishwa na watangulizi wake, badala yake atumie sheria na kanuni zilizopitishwa, kuhakikisha anavifutia usajili viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kushindwa kuendeleza uzalishaji kwa muda mrefu sasa ambavyo vimegeuka kuwa maficho ya wanyamapori.

Dk Magufuli alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi katika Kata ya Maweni jijini Tanga wakati wa sherehe za kuweka jiwe la ufunguzi wa kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro. Kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro kinachozalisha saruji ya kiwango cha 32.5N na 42.5N, ujenzi wake ulianza mwaka 2013 kinatarajiwa kuzalisha tani 3,000 kwa siku, ambapo kwa sasa uzalishaji ni tani 800 na kimejiari wafanyakazi 189.
“Hivi wewe waziri mwenye dhamana kwa nini kila wakati nasikia na kuona viwanda mbalimbali vikifunguliwa, lakini nashangaa kwa sababu sijasikia viwanda visivyozalisha vikifutwa kama anavyofanya mwenzako wa Wizara ya Ardhi kufuta hati za umiliki wa ardhi za mashamba mkubwa? Sasa nakuomba kwa mara ya mwisho hebu fumba macho na uwakung'ute,” alisema Dk Magufuli na kuongeza: “Mimi ndiye niliyekuteua kushika dhamana hii ya viwanda na biashara, sasa unaogopa nini? Kuanzia sasa nataka nisikie watu wamenyang'anywa, hatuwezi kuendelea kuacha maeneo hayo ya wananchi ambayo watu wameuziwa kwa bei mdogo na kuyatelekeza “Nenda kawatoe, usijali hata kama mmiliki ni kutoka CCM wewe nyang'anya, ikiwa ni mwanachama wa CUF, Chadema awe ni waziri au mbunge wewe nyang'anya.
Hawatakufanya jambo lolote hatuwezi kuendelea kuruhusu jambo hili liendelee.” Alifafanua, “Nchi hii imechezewa sana, viwanda hivi vilikuwa ni mali ya Watanzania na wenzetu waliovinunua wameamua kuviua. Kwa mfano, hapa Tanga kwenye taarifa yenu hapa imeeleza kwamba kuna viwanda kumi na mbili vilivyobinafsishwa vyote havifanyi kazi, sasa wakati umefika kwamba lazima viwanda virejeshwe serikalini ili wakuu wa mikoa wakabidhi wawekezaji wengine wanaohitaji kufanya uzalishaji.”
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, nchi nzima ina viwanda 197 vilivyotelekezwa baada ya kubinafsishwa takribani miaka 20 iliyopita, vikiwemo viwanda vilivyopo mkoani Tanga. Aidha, Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha wanatembelea na kufanya tathmini ya viwanda vyote vya serikali vilivyoko katika maeneo yao, ambayo kwa sasa havifanyi uzalishaji na kuwasilisha orodha na mapendekezo ya kuvifuta ili waziri aweze kuwanyang'anya wamiliki.
Akizungumzia kiwanda hicho cha saruji cha Kilimanjaro kitakachozalisha tani 3,000 kwa siku baada ya ujenzi kukamilika, aliwapongeza wawekezaji hao kwa kutoa huduma kwa jamii na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuingiza kwenye mpango wa halmashauri barabara yenye urefu wa kilometa 3.5 inayoingia kiwandani hapo ili kuwapunguzia mzigo wa gharama za ukarabati.
“Kwa kuwa hawa ni wawekezaji wazalendo, hawadaiwi kodi na wameweza kutia mifuko 1,300 ya saruji kusaidia ujenzi wa zahanati, madarasa katika kata hii ya Maweni, basi nami nakuagiza mkurugenzi hii barabara iweke kwenye mipango ya halmashauri kwa kutumia bajeti ya mfuko wa barabara ili kiwanda kitumie fedha hizo kuongeza mishahara ya wafanyakazi,” alieleza Dk Magufuli.
Tanzania kwa sasa ina jumla ya viwanda 11 vyenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 10 za saruji kwa mwaka, wakati mahitaji ya sasa ya bidhaa hiyo ni wastani wa tani milioni 4.7. Baada ya kufungua kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga (Tanga Fresh), ambacho kinatarajia kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 50,000 kwa siku hadi kufikia lita 120,000, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya wafugaji kutoka 6,000 hadi 12,000.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na vyama vya ushirika vya wafugaji 24 kwa asilimia 42 na mwekezaji kutoka Uholanzi kwa asilimia 58 na upanuzi unaofanywa, utaongeza uwekezaji kutoka Sh bilioni 12 hadi kufikia Sh bilioni 26.5. Akiwa kiwandani hapo, ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukabidhi hati miliki ya kiwanda hicho kwa menejimenti ya kiwanda, na ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyokuwa ikidai kodi ya ongezeko la mtaji kuelekeza madai hayo kwa mmiliki wa awali wa kiwanda hicho, aliyewauzia wakulima.
Rais Magufuli amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuchukua hatua dhidi ya kiwanda cha maziwa cha Arusha ambacho baada ya kubinafsishwa, kimegeuzwa kuwa kituo cha kukusanyia maziwa na kuyasafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kusindikwa. Pia amemwagiza Mwijage kuwa nchi yoyote itakayozuia maziwa ya Tanzania, nayo izuiwe kuingiza maziwa yake nchini.
Aidha, ametoa siku tano kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kufika kiwandani hapo na kushughulikia changamoto zinazokikabili kiwanda hicho. Rais Magufuli pia amefungua awamu ya kwanza ya mradi wa kituo cha matangi ya mafuta cha GBP kilichopo katika eneo la Raskazone, Tanga ambacho kina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 122.6 na ambacho kinatarajia kupanuliwa hadi kufikia lita milioni 300 ifikapo katikati ya mwaka ujao.
Dk Magufuli alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa GBP, Badar Sood kwa uwekezaji huo mkubwa wa Sh bilioni 60 utakaojumuisha ujenzi wa kiwanda cha vilainishi na kiwanda cha kusindika gesi na amemhakikishia kuwa serikali itaendelea kumuunga mkono wakati wowote. Pia Rais Magufuli alimpongeza Sood kwa kulipa kodi ipasavyo, ambapo katika miaka miwili iliyopita ameongeza malipo ya kodi kutoka Sh bilioni 208.950 hadi kufikia Sh bilioni 293.263 na aliwahakikishia wawekezaji wote wanaolipa kodi ipasavyo kuwa wapo salama na serikali itawalinda. Rais Magufuli alielezea kutoridhishwa kwake na kusuasua kwa mchakato wa ununuzi wa mita za kupimia mafuta, yanayoshushwa kutoka melini.