Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wafanyabiashara wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wanaodaiwa, kulipa madeni kabla ya Septemba 30, mwaka huu.

Amesema kwa wale watakaoona hawawezi kulipa madeni yao hadi Septemba 30, ni vyema wakaondoka wenyewe ili kuwaachia watu wengine nafasi, kwa kuwa kodi mbalimbali zinazokusanywa zinatumika katika kuboresha huduma mbalimbali katika uwanja huo.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo katika mkutano wake na wafanyabiashara mbalimbali wanaofanya shughuli zao katika uwanja huo, ambapo pia amesema ili serikali iweze kuboresha huduma mbalimbali ni lazima wafanyabiashara hao walipe gharama zote, ikiwemo kodi za pango na kodi zingine.