Baadhi ya Mahujaji wakiwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
NI karibu saa 72 sasa, mahujaji takribani 100 wanasota katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), huku wakikabiliwa na mateso mbalimbali, baada ya taasisi zilizotakiwa kuwasafi risha kushindwa kufanya hivyo.

Hadi jana jioni gazeti hili lilishuhudia mahujaji hao wakiendelea kusota katika kiwanja hicho cha ndege wakisubiri hatima ya safari hiyo ya kwenda kufanya ibada ya Hija. Mahujaji hao ambao walitakiwa kuondoka juzi jioni kwenda kufanya ibada hiyo katika Mji Mtakatifu wa Makkah, Saudi Arabia hawakuweza kuondoka huku baadhi yao wakilala uwanjani hapo kutokana na kutoka mikoani.
Taasisi zilizotakiwa kuwasafirisha mahujaji hao ni Taiba Hajj & Umrah Social Service Trust na Jamarat Hajj and Umrah Traveller, ambazo hata viongozi wake hawakuwa wakipatikana kwenye simu.
Wakizungumza na HabariLeo kwa nyakati tofauti, mahujaji hao wamelaani kitendo kilichofanywa na viongozi wa taasisi hizo mbili, kwa kuwa wamekatisha ndoto zao za kwenda kufanya ibada hiyo muhimu.
“Kilichotokea kimetusikitisha wananchi na Waislamu wote kwa ujumla, ilitakiwa tusafiri leo lakini mpaka dakika hii viongozi wamekimbia, hawapokei simu wala hawatufahamishi chochote kinachoendelea, pasipoti zetu wanazo na tiketi wamezizuia,” alisema Ummy Sekibo.
Ummy alisema, viongozi wa dini na serikali wanatakiwa kuzichukulia hatua taasisi za aina hiyo, kwa kuwa si mara ya kwanza kufanya kitendo hicho cha kukusanya fedha za mahujaji na kushindwa kuwasafirisha.
Alisema watu wamejinyima na kuweka fedha kwa muda mrefu kwa ajili ya kwenda kufanya ibada hiyo, lakini taasisi hiyo imechukua fedha zao na kuingia mitini. “Hii ni dhuluma na wamebeba dhima, wamechukua hela za watu, watu wamejinyima, wamejidhiki kila siku toka tarehje ishirini na tatu wanatuambia tunasafiri... binafsi nimejinyima nasema naenda kufanya ibada lakini hii si ibada tunachofanya tunajikalifisha nafsi zetu na tunapata dhambi,” alisema.
Hussein Seif ambaye ni mkazi wa Mwanza alisema kitendo hicho kimewaumiza kwa kuwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa kitabu kitakatifu cha Quran, lakini wameshindwa kukamilisha ibada hiyo na wakiwa hawajui waelekee wapi.
Alisema alilipa Sh milioni 8.5 kwa taasisi ya Taiba Hajj & Umrah Social Service Trust, lakini ameshindwa kusafiri na kushauri taasisi hiyo ifungiwe ili waislamu wengine wasije kufanyiwa kitendo hicho.
“Huwezi kukusanya mamilioni ya hela, halafu huna mpangilio ulio sahihi, tunadhalilisha dini yetu sisi, hizi taasisi ni bora zifungiwe, bora iwepo taasisi moja yenye ukweli, hali ni ngumu sasa hivi, natoa milioni nane niende Hija halafu sifanikishi,” alisema Seif.
Hata hivyo, Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir aliwataka mahujaji hao kuwa na subira kwa kuwa wanaendelea kuwatafuta viongozi wa taasisi hizo ili kuhakikisha wanaondoka na kwenda kutekeleza ibada hiyo.
“Cha msingi tustahimili, tuswali na mimi nitaendelea kufuatilia kuona kwamba safari inakamilika kupitia viongozi...lakini bado muda mzuri, wasiwasi wangu nilikuwa najaribu kufuatilia nilifikiri labda leo saa sita (juzi) ndio inafungwa mipaka lakini itafungwa kesho (jana) kuamkia Jumapili,” alisema Mufti.
Aliwataka mahujaji hao kufanya ibada na kuomba dua ili waweze kusafiri kwenda Makkah waweze kutekeleza ibada hiyo muhimu. Mara kwa mara Mufti Zubeir amekuwa akiwasisitizia waislamu kutumia Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) katika safari za kwenda hija kutekeleza ibada hiyo muhimu.
Ibada ya Hija ni nguzo ya tano katika nguzo za Uislamu. Nguzo nyingine ni kutamka shahada mbili, kusali swala tano, kutoa zaka na kufunga mwezi wa Ramadhani.