MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za kifedha pamoja na benki kuwa na masharti mepesi na maalumu ya mikopo kwa wanawake wajasiriamali wadogo.
Amesema inashangaza kuona riba kubwa kwenye mikopo lakini kwenye amana riba, ikiwa ni ndogo na kuagiza uongozi katika benki zote nchini, kufanya kazi kwa maendeleo ya watu wote.

Katika hatua nyingine, Samia amewataka wanawake kutumia mazingira wezeshi na fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi, na kuachana maneno yasiyo na tija. Alitoa mwito huo jana alipokuwa akizindua Jukwaa la Uwezeshaji la Wanawake la Dar es Salaam, tukio ambalo lilienda sambamba na uzinduzi wa Mfumo Maalumu wa Akaunti wa Benki ya CRDB.
Kuhusu mikopo, Makamu wa Rais aliziagiza taasisi za kifedha pamoja na benki kurekebisha mifumo yao ili kuwa na masharti mepesi na maalumu ya mikopo kwa wanawake wajasiriamali wadogo.
“Inashangaza kuona riba kubwa kwenye mikopo lakini kwenye amana riba ni ndogo, niwaombe watu wa benki tufanye kazi kwa maendeleo yetu sote,” alisema. Aidha alisema umoja na mshikamano kwa wanawake, ndio ngao pekee ya kupigana katika uchumi, hivyo wanawake wajiunge katika umoja huo na kutumia fursa kwa pamoja.
Samia alitaka pia iandaliwe taarifa ya majukwaa hayo, ambayo mpaka sasa yameanzishwa katika mikoa 23 nchi nzima, wapi kuna mafanikio, palipokwama na pia mahitaji na pia amehamasisha mikoa ambayo haijaanzisha majukwaa hayo kuanzisha.
“Madhumuni ya majukwaa haya ni kuwawezesha kiuchumi lakini wanawake tuache ujike, maneno maneno, kuzodoana, tuaminiane na ikitokea mwanamke mwenzetu kapata nafasi tumpe nguvu twende pamoja,” alisema Samia.
Aliyataka majukwaa hayo ya wanawake pamoja na mambo mengine, kuisimamia serikali kwa kufatilia fedha zinazotengwa kwa ajili yao na pia wawe na utaratibu mzuri wa kutunza fedha zao. Samia aliwaasa watanzania kuthamini bidhaa za ndani ili kukuza soko la bidhaa hizo.
Mwenyekiti wa Jukwaa hilo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema wanawake ndio ambao wataitoa nchi hii kwenye umasikini. “Kufikia mwaka 2020 tuwe tumewawezesha kina mama waliojipanga kushiriki katika Tanzania ya viwanda, na tunaamini tunaweza,” alisema Mjema.
Mjema alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam wamejipanga wanawake kuzalisha bidhaa mbalimbali, kulingana na eneo husika ili kuhakikisha inasaidia pia katika upatikanaji wa masoko.
Alisema atahakikisha jukwaa hili linashuka ngazi ya wilaya mpaka kata na hakuna mwanamke ambaye ataachwa nyuma huku akizitaka benki kufungua kanda maalum za kibenki kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanawake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema ni wakati sasa wanawake kutambuliwa na kuwezeshwa na kupata fursa ya kujenga uchumi wao.
Alisema sera iliyopo sasa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ina nguzo tisa, ambazo ni pamoja na kuboresha mifumo na sheria, kuwajengea ujuzi na kuimarisha ushiriki katika rasilimali zilizopo.
“Sera hiyo haina budi kuwawezesha wanawake wote, majukwaa haya tunaamini yatatoa fursa kwa wote,” alisema Jenista. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Charles Kimei alisema majukwaa hayo, yawasaidie wanawake kujadili fursa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutumia benki kuongeza mitaji yao.
Alisema kuanzishwa jukwaa hilo kutasaidia kuharakisha kufikia malengo endelevu 2030 na Azimio la Beijing na mikataba mbalimbali, ambayo kama nchi imeridhia katika kuwasaidia wanawake.
“Niwaombe wanawake kutumia kikamilifu majukwaa haya katika kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na pia kutumia fursa zilizopo,” alisema. Alisema wizara mama hiyo itaendelea kushiriki kuratibu majukumu kuhakikisha wanawake wanashiriki na kunufaika na maendeleo ya uchumi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wajasiriamali Wanawake nchini (TWCC), Jacqueline Maleko alisema chama hicho mpaka sasa kimepata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wanawake wajasiriamali mipakani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga aliwataka wanawake kujiunga katika TWCC kwani kuna fursa nyingi ambazo zina lenga kuwakwamua wanawake kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Uwezeshaji Tanzania (NEEC), Ben Issa alisema wameweza kuanzisha majukwaa 23 katika mikoa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na la Dar es Salaam lililoanzishwa jana.