Kijana mwenye umri wa miaka 23 ambaye alikuwa mgombea wa kujitegemea katika uchaguzi huu ndiye atakuwa mbunge mpya wa Igembe Kusini, katika kaunti ya Meru mashariki mwa jiji la Nairobi.
John Paul Mwirigi ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu Somo la Ualimu katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 18,867 na kumshinda mpinzani wake wa karibu Rufus Miriti wa chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta, ambaye alikuwa na kura 15,411.
Wagombea wengine, ambao wamekuwa wanasiasa kwa muda mrefu ni Mwenda Mzalendo aliyepata kura 7,695, Kubai Mutuma (6,331) na Raphael Muriungi (2,278).
Bw Mwirigi, ambaye huenda akawa mbunge mwenye umri mdogo zaidi kuchaguliwa baada ya uchaguzi huo wa Jumanne hakuwa na kampeni yenye madoido na pesa.
Alisema kuwa alikuwa akipiga kampeni kwa kutembea kwa miguu kutoka nyumba moja hadi nyingine kabla ya kupata msaada kutoka kwa wahudumu wa boda boda.
Wafuasi wake walianza kusherehekea Jumatano wakati matokeo ya awali yalionyesha kuwa alikuwa mbele ya wapinzani wake.
Akizungumza na gazeti la 'Daily Nation' Bw Mwirigi alisema alianza kuvutiwa na siasa akiwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Kirindine.
"Niliota nilikuwa nikitoa hoja katika bunge wakati nilikuwa kidato cha tatu. Ndio wakati nilianza kuwauliza wanafunzi wenzangu kunifanyia kampeni kwani ningehitaji kura zao mwaka 2017. Nimeshikilia nafasi za uongozi shuleni na nyumbani," alisema Bwana Mwirigi.
Mwirigi alisema ajenda yake ya kwanza itakuwa kusaidia shughuli za biashara ya kilimo, kukuza ujasiriamali na kulea vipaji.
"Kwa kuwa mimi ninatoka kwenye familia maskini, ninaelewa maswala yanayoathiri wakazi. Ajenda yangu muhimu itakuwa kubadilisha maisha ya watu," anasema.
Bw Mwirigi wa sita katika familia ya watoto wanane anasema bado anaishi katika 'ghala' na hamiliki shamba lolote, kinyume na madai ya kuwa aliuza shamba lake kwa ajili ya kampeni.
Wakazi wanasema wameamua kumchagua kijana huyo licha ya yeye kukosa rasilimali kwa sababu wana uhakika anayafahamu vyema matatizo yao na atayashughulikia.
0 Comments