WINGA wa Klabu ya Azam FC Joseph Kimwaga akiwa katika chumba cha matibabu katika Hospitali ya Vincent Palloti iliyopo jijini Cape Town nchini Afrika Kusini.
WINGA wa Klabu ya Azam FC Joseph Kimwaga, anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda miezi minne baada ya kubainika ya kuwa amechanika mtulinga wa kati ‘meniscus’ kwenye goti lake la mguu wa kushoto.
Kimwaga hivi sasa yupo nchini Afrika Kusini tokea Ijumaa iliyopita akifanyiwa matibabu ya goti lake hilo, aliloumia wakati Azam FC ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda ulioisha kwa matajiri hao kushinda bao 1-0 wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, aliyeambatana na Kimwaga nchini humo, amesema kuwa mchezaji huyo alifanyiwa vipimo jana Jumatatu na Dr. Nickolas kwenye Hospitali ya Vincent Palloti iliyopo jijini Cape Town nchini humo.
“Jumatatu (4/9/2017)alifanyiwa vipimo na kuthibitika amechanika Meniscus upande wa kati pia
ameumia mtulinga wa kati ACL(Anterior Cruciate Ligament),” alisema kwenye ripoti aliyoipokea kutoka kwa Dr. Nickolas.
Mwankemwa alisema baada ya kufanyiwa kipimo hicho, Kimwaga anatarajiwa kulazwa kesho Jumatano saa 9.00 Alasiri, huku akitarajiwa kufanyiwa upasuaji mdogo (athroscopy) siku inayofuata Alhamisi kabla ya kutoka hospitalini Septemba 9 mwaka huu na kurejea nchini siku nne baadaye (Septemba 13) .
Amesema Upasuaji wa kwa njia ya Athroscopy ni ule wa kisasa kabisa ambao wataalamu hutumia vifaa maalum, ambavyo huingizwa kwenye goti ambavyo hufanya matibabu na kuondoa matatizo yote katika eneo hilo, faida yake humfanya mchezaji kurejea mapema uwanjani kuliko ule wa kupasuliwa goti zima.
Winga huyo mara baada ya kufanyiwa upasuaji Alhamisi anatarajiwa kukaa nje ya dimba kwa kipindi cha miezi minne kutoka siku ya upasuaji.
Azam FC inamtakia kila kheri Kimwaga katika matibabu yake hayo, yaweze kwenda salama kama yalivyopanga na hatimaye aweze kurejea dimbani mapema. |
0 Comments