Watahiniwa 917,030 kutoka shule za msingi 16,581, za Tanzania Bara wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE 2017) Septemba 6 hadi 7 , mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI George Simbachawene amesema kuwa maandalizi ya uendesheji na usimamizi wa mtihani huo yamekamilika katika ngazi zote ikiwemo kusafirishwa kwa mitihani na wasimamizi kutoka ngazi ya Halmashauri kwenda kwenye vituo vya kufanyia mtihani.
“Jumla ya shilingi , 29,474,964,600 zitatumika kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na usimamizi wa mtihani huo kwenye mikoa na Halmashauri” ameongeza George Simbachawene.
Aidha, Waziri Simbachawene amewataka viongozi wa Serikali kushirikiana kwa hali na mali na kuhakikisha zoezi hilo muhimu na nyeti linafanyika kwa utulivu na ufanisi kwa kuwataka wanajamii wote, wazazi na walezi wawaruhusu wanafunzi kuhudhuria na kufanya mtihani huo kwa amani.
“Ndugu walimu, jiepusheni na udanganyifu au kusaidia kutekeleza udanganyifu. Natoa wito kwenu mkasimamie vema vijana wetu ili waweze kufanya mtihani wao kwa usalama haki na usawa ili tuweze kuwapata vijana watakaojingana kidato cha kwanza wenye sifa zinazostahili na si vinginevyo” amesisitiza Simbachawene.
Waziri Simbachawene amewaagiza viongozi wanaohusika na mtihani huo kuanzia ngazi za mikoa na Halmashauri wahakikishe wanakamilisha kwa wakati upelekaji wa mitihani na vifaa kulingana na mahitaji kwa wakati. |
0 Comments