MAKAMU wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa jitihada za kufanikisha mtangamano na maendeleo endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki hazina budi kuainishwa na juhudi za kuhimiza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana.

Samiya aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Kongamano la kwanza la Kimataifa la siku mbili huko Hoteli ya Golden Tulip Malindi Visiwani Zanzibar. Amesema kuwa uteuzi wa Kiswahili kuwa luha ya mawasiliano mapana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umeweka mazingira muafaka ya utengamano wa kikanda kuliko wakati mwengine wowote katika historia ya ukanda huu. "Sote ni mashahidi wa namna lugha inavyokuwa na nafasi kubwa katika suala zima la mtangamano pamoja na kuleta maendeleo, mustakbali wa jumuiya hii unahitajika mikabala mipya iliyovuka ile ya kimapokeo iliyojifunga tu katika ushirikiano wa kimasoko’’, alisema.
Hivyo amesema kuwa hadhi ya sasa ya Kiswahili kikanda na kimataifa inaagiza kuwepo kwa mageuzi, mrekebisho na uwezeshaji wa lugha hiyo, ambapo amesema ili kufanikisha jukumu hilo la kipekee, maendeleo na matumizi ya Kiswahili sharti yapangwe, yaratibiwe na yaendelezwe kimkakati.
Sambamba na hilo Samia alitumia fursa hiyo kuipongeza Kamisheni ya Kiswahili kwa kutambuwa hilo na kuandaa mpango mkakati wake wa kwanza ili kutoa mwelekeo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo mpango ambao alisema huu ni muongozo mzuri wa namna Kamisheni itakavyotumia mamlaka kutekeleza majukumu yake katika mazingira yanayokubadilika ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Aidha alisema kuwa wanapaswa kuiga mfano kikamilifu katika juhudi za kamisheni za kuendeleza kwa ufanisi matumizi ya Kiswahili katika utangamano na katika maendeleo endelevu ya Jumuiya hiyo. Hata hivyo amesema kuwa Kiswahili kimekuwa kiunganishi na kimetumika katika utangamano wa kiknda tangu zamani hata kabla ya ukoloni ambapo amesema kuwa kilikuwa kilitumiwa na watu katika safari, biashara, huduma na kubadilishana mawazo.
Amesema kuwa kinyume na mikabala ya awali Jumuiya ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya kiuchumi, juhudi za sasa zinaongozwa na uhalisia wa kiutendaji unaofangamana na mahitaji na utashi wa kimataifa na wa kikanda ngazi zote za jamii ili kuimarisha ushirikiano wa pamoja. Aidha amesema kuwa Serikali za Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zitajitahidi kuhakikisha kwamba wanatimiza wao wa kuiwezesha kamisheni kutekeleza mapendekezo ya kisera yatakayotoewa.