|
MAANDALIZI ya Kongamano la kwanza la Kiswahili la kimataifa, lililoandaliwa na Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki, yamekamilika na linatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia kesho mjini Zanzibar.
Limelenga kutoa fursa ya kujadiliana juu ya maendeleo na matumizi ya Kiswahili, yanavyoweza kuchochea uibukaji wa mawazo mapya, na utatuzi wa matatizo na upatikanaji wa suluhu za changamoto za maendeleo endelevu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamisheni hiyo, mada kuu katika kongamano hilo inatarajiwa kuwa “Kuleta Mabadiliko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki Kupitia Kiswahili”. Kutakuwa pia na mada ndogo zikiwemo “Kiswahili, Mfungamano wa Kikanda na Maendeleo”, “Kiswahili na Upatikanaji wa Rasilimali”, “Kiswahili, Kujua Kusoma, Kuandika na Afya”, “Kiswahili, Biashara na Kazi”, Kiswahili, Elimu na Mabadiliko”, “Kiswahili, Siasa na Demokrasia” na “Kiswahili, Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi”.
Nyingine zitahusu “Kiswahili na Mabadilliko ya Tabia Nchi”, “Kiswahili, Vyombo vya Habari na Mawasiliano kwa umma” na “Kiswahili, Utandawazi na Ushirikiano wa Maendeleo.”
Taarifa hiyo ilisema kongamano hilo, litawakutanisha watungaji na watekelezaji sera, washirika wa maendeleo, wataalamu wa tasnia ya habari, wanazuoni na wadau wengine wa Kiswahili, na kutoa fursa ya kutafakari kwa pamoja kuhusu namna Jumuiya ya Afrika Mashariki inavyoweza kukua na kubadilika kupitia utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo.
Imesema hilo jambo ni muhimu kwa uthabiti na maendeleo ya kikanda katika mazingira yanayobadilika kwa kasi yakiambatana na ugunduzi na mageuzi mapya. Ubunifu, uvumbuzi na mbabadiliko katika maendeleo sambamba na matumizi ya Kiswahili kwani ni mambo yenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha maarifa, stadi na mielekeo stahiki katika kukabiliana na changamoto za Malengo Endelevu ya Maendeleo.
“Malengo Endelevu ya Maendeleo yanakipa Kiswahili nafasi muhimu ya kusaidia katika kutatua changamoto za maendeleo zinazokabili Jumuiya ya Afrika Mashariki. “Kongamano hilo limejengwa katika dhana kwamba ajenda ya maendeleo ya baada ya 2015, itakuwa na athari kubwa kisera, kimipango na kiutekelezaji duniani kote kwa miaka 15 ijayo.
Kila lengo la Malengo Endelevu ya Maendeleo linatoa fursa ya mawasiliano kwa kutumia Kiswahili. Malengo na shabaha zake zinatoa fursa kubwa kwa Kiswahili ya kudhihirisha umuhimu wake, na wakati huohuo kikitoa mchango katika ukuaji endelevu wa kitaifa na kikanda.
“Lengo la Kongamano hili ni kutoa fursa ya kujadiliana kuhusu jinsi maendeleo na matumizi ya Kiswahili yanavyoweza kuchochea uibukaji wa mawazo mapya, na utatuzi wa matatizo na upatikanaji wa suluhu za changamoto za maendeleo endelevu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
0 Comments