MWANAMITINDO Amisa Mobeto amemfungulia mashtaka msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ katika Mahakama ya watoto Kisutu, Dar es Salaam.
Mwanamitindo huyo ni mzazi mwenza wa Diamond ambapo mwaka huu wamepata mtoto wao wa kiume, lakini katika siku za hivi karibuni wawili hao wamekuwa wakipishana kauli zao.

Nakala ya hati ya wito wa mahakamani iliyotumwa kwa Diamond ambayo gazeti hili limeiona jana, imemtaka msanii huyo kufika mahakamani Oktoba 30 mwaka huu asubuhi. Katika hati hiyo pia msanii huyo ametakiwa kuwasilisha nyaraka zake muhimu ambazo anaona zitamsaidia katika kesi hiyo huku akitakiwa kutokosekana mahakamani siku hiyo.
Hamisa amefungua madai katika mahakama hiyo akidai pamoja na mambo mengine, Diamond amemkashifu na hajamwomba radhi akitaka matunzo ya mtoto wao mchanga kwa Diamond.
Akihojiwa na kipindi cha Leo Tena cha Clouds Tv hivi karibuni, Diamond alikiri kuzaa na Hamisa mtoto huyo na kumwomba radhi mzazi mwenzake, Zari akisema yuko tayari kutembea kwa magoti hadi Afrika Kusini kuonesha masikitiko yake kwake.
Pia alisema amekuwa akimpa Hamisa Sh 500,000 kila mwezi za matunzo ya mtoto huyo na amemnunulia mwenza huyo gari na akashangaa kwa nini analalamika wakati fedha hizo ni nyingi.
Nakala hiyo ya wito wa kuitwa mahakamani ilitolewa Oktoba 4 mwaka huu na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama hiyo. Nakala hiyo ya Diamond kuitwa mahakamani imetolewa siku moja baada ya msanii huo kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Katika sherehe hiyo, Diamond alitoa misaada mbalimbali katika Hospitali ya Amana, Ilala na kufuatiwa na hafla ya kifahari katika hoteli ya nyota tano ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Dar es Salaam.