Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akihutubia jukwaa la biashara mkoni Shinyanga.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wananchi wa Shinyanga kujiandaa kupokea fursa mpya zinazojitokeza ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta litakalopita Shinyanga kutoka Uganda hadi Tanga.
Aliyasema hayo jana wakati akifungua rasmi Jukwaa la Biashara mkoani Shinyanga lililoandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

TSN ndiyo mchapishaji wa magazeti ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo. “Tuna tatizo la fursa zinatokea katika maeneo yetu kutupita hivi hivi na badala yake kuchukuliwa na wageni,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza kuwa wakazi wa Shinyanga wasipojiandaa, watajikuta fursa nyingi zinazotangazwa na kuibuliwa zikichukuliwa na wageni wakiwemo hata kutoka nje ya nchi.
Shinyanga iko jirani na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya. Alitoa mfano kwamba wakati gesi ilipoanza kutafutwa na kuchakatwa mkoani Mtwara, baadhi ya wageni walilazimika kuruka kwa ndege kwenda kulala Mkoa wa Kilimanjaro na kurejea asubuhi.
“Lakini sasa Mtwara wamegeuza changamoto hiyo kuwa fursa. Ukienda Mtwara sasa utaona kuna hoteli kubwa,” alisema. Aliwataka wananchi wa Shinyanga kuandaa vijana wenye ujuzi kwa ajili ya viwanda na hata vibarua pale bomba la mafuta litakapopita Shinyanga wakiwemo mama lishe wenye vifaa vya kutosha.
Dk Mwakyembe aliipongeza TSN kwa kubuni Jukwaa la Biashara ambalo limekuwa likiwakutanisha wadau mbalimbali, wakakaa wakijadili fursa za maendeleo na kwamba kila lilipofanyika limeacha mtazamo chanya kuhusu maendeleo ya kiwanda husika.
Jukwaa lililofanyika jana Shinyanga ni la nne, la kwanza likifanyika Februari mkoani Simiyu, la pili lilifanyika Aprili jijini Mwanza na la tatu likafanyika mwezi uliopita jijini Tanga. Aliitaka TSN kuendelea kuutangaza Shinyanga katika vyombo vyake vya habari vya magazeti na mitandao ili Watanzania wazijue vema na fursa zake.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack wakati akimkaribisha mgeni rasmi, alisema mkoa wake una fursa za uwekezaji katika madini, ardhi, kilimo na ufugaji. Alisema kutokana na mkoa kuwa na neema ya madini ya dhahabu na almasi, anawakaribisha wawekezaji mkoani Shinyanga kufungua viwanda vya kuongezea thamani mazao hayo ya almasi na dhahabu kwa maana ya kuzalisho vito kama mikufu, vidani na kadhalika.
Baadhi ya wadau wa maendeleo walioshiriki kudhamini Jukwaa hilo ni Benki za NMB, TIB Corporate na TIB Development. Wadhamini wengine ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Watumishi Housing Corporation, Benki ya Wanawake (TWB), Karena Hotel, MarLink na Jambo Industries.