SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema ujumbe wa viongozi wa Serikali ya Oman uliokuja nchini na kukutana na Rais John Magufuli na wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein haukuwa na malengo ya kisiasa, bali ulilenga zaidi kuimarisha masuala ya uchumi na maendeleo na kuitangaza sekta ya utalii.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alisema hayo jana wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana katika ziara ya ujumbe wa Serikali ya Oman wiki hii. Aboud alisema ujumbe huo ulikuja kwa agizo la Sultani Sayid Qaboos bin Said Al Said kuimarisha uhusiano uliopo wa muda mrefu na kuangalia fursa za kiuchumi na maendeleo za kuisaidia Zanzibar.
Alisema Serikali ya Oman imekubali kulifanyia ukarabati mkubwa Jengo la Bait-al-Jaib lililopo Mji Mkongwe wa Zanzibar na kulirudisha katika hadhi yake ya asili kwa ajili ya kukuza sekta ya utalii. Alisema Oman ipo tayari kugharamia ujenzi huo na kinachosubiriwa ni kupitiwa michoro ya ujenzi wa jengo na Kitengo cha Miji ya Kale kilichoko urithi wa kimataifa ambacho ujumbe wake uko Zanzibar.
Timu ya kitengo cha Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inayoshughulikia miji iliyopo katika urithi wa kimataifa, ilikuwepo Zanzibar wiki hii kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kufanya tathmini ya kuwekeza katika majengo matatu yaliyopo Mji Mkongwe.
Aidha, Waziri huyo wa SMZ alisema Serikali ya Oman imekubali kusaidia kazi za utafiti wa nishati na mafuta kutokana na kuwepo kwa taarifa za Zanzibar kuwa na dalili za kupatikana kwa mafuta.
Ujumbe wa Oman ulioongozwa na Waziri wa Mafuta na Gesi, Dk Mohamed Hamad Al-Rumhy ulipata nafasi ya kuzungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na ulipokuwa mjini Dar es Salaam, ulifanya mazungumzo na Rais John Magufuli na kuwasilisha ujumbe kutoka kwa Mfalme Qaboos. Zanzibar ilitawaliwa na utawala wa Sultani kutoka Oman hadi utawala huo ulipopinduliwa na wananchi wazalendo kushika hatamu ya kuongoza dola Januari 12, 1964.
|
0 Comments