BAADHI ya wanafunzi wa shule za Sekondari nchini wameiomba Wizara ya Elimu kupunguza idadi ya masomo kutoka manane hadi matano ili wamudu vizuri na kufaulu vizuri mitihani.
Mwanafunzi Issa Juma wa shule ya sekondari ya Bambi wilaya ya Kati Unguja alisema masomo wanayofanyia mitihani ni mengi. Alisema wanapata wakati mgumu kusoma yote kwa wakati mmoja huku wakitakiwa kufanya mitihani ya taifa ya kidato cha nne hadi cha sita. Fatuma Jaku, mwanafunzi wa shule ya Pagali wilaya ya Kati Unguja aliomba wizara kupanga masomo muhimu katika mitihani ya kitaifa.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri alisema wizara ipo katika mikakati ya kuimarisha maabara katika shule na kuajiri wafanyakazi wa kuzisimamia. Alisema imebainika lipo tatizo la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi ikiwemo ufaulu mdogo wa wanafunzi katika masomo hayo. Alisema mikakati ya Wizara ya Elimu kwa mwaka wa fedha wa bajeti 2017-2018 ni kuimarisha shule kwa kuzipa madawati na kuimarisha maabara zake kwa vifaa vya sayansi.
|
0 Comments