MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dodoma jana ilimwachia kwa dhamana aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Taifa (UVCCM), Sadifa Juma Hamis (35) anayekabiliwa na tuhuma za rushwa.
Sadifa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 11, mwaka huu na kukataliwa dhamana baada ya upande wa mashtaka kudai akiwa nje kwa dhamana ataingilia uchaguzi wa UVCCM taifa uliokuwa ukiendelea wakati huo na kuingilia uchunguzi uliokuwa ukifanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma shauri hilo jana la uamuzi mdogo kuhusu dhamana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Fovo alisema vigezo ambavyo vilitolewa na wakili wa serikali havihusiani kwa namna yoyote kuvuruga uchunguzi na kuingilia upelelezi kama ambavyo walidai upande wa mashtaka.
Alisema mshitakiwa anaruhusiwa kudhaminiwa kwani ni haki Kikatiba kutokana na kifungu namba 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakimu Fovo alisema mazingira ya kesi hiyo na vigezo vilivyotolewa na wakili wa serikali ni tofauti kabisa hivyo haoni sababu ya kumnyima dhamana mshtakiwa.
Alidai kuwa Kifungu cha 15 (i) (b) walichokitumia mawakili wa serikali kwa kuzuia dhamana kwa mtuhumiwa hakimzuwii mtu yeyote kupewa dhamana hivyo sababu za upande wa Jamhuri hazikuwa na mashiko.
Mshtakiwa aliachiliwa huru baada ya masharti ya dhamana aliyopewa ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini fungu la dhamana la Sh milioni moja kila moja. Mshtakiwa alitimiza masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru hadi Januari 18, mwakani kesi yake itakapotajwa tena.
Mshtakiwa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge Zanzibar alifikishwa mahakamani Desemba 11, mwaka huu akikabiliwa na mashtaka ya rushwa. Awali, ilidaiwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Biswaro Biswaro kuwa katika kesi hiyo ya jinai namba 232 ya mwaka 2017, mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 9, mwaka huu akiwa nyumbani kwake maeneo ya Kata ya Mnadani Manispaa ya Dodoma.
Alisema katika kosa la kwanza Sadifa anadaiwa kuwa akiwa nyumbani kwake alitoa rushwa ya vinywaji kwa wajumbe ili wamchague mgombea wa nafasi ya Makamu mwenyekiti wa UVCCM, Rashid Mohamed Rashid.
Biswaro alisema kosa la pili analokabiliwa nalo Sadifa ni kutoa ahadi ya kuwalipia gharama za usafiri wajumbe hao kutoka Dodoma– Kagera kama zawadi kwao baada ya kumpigia kura mgombea huyo.
Wakili huyo aliwataja wajumbe hao kuwa ni Kadogo Shabani, Abdallah Hamimu, Octavian Andrea, Didas Zimbihile, Tasinta Nyamwiza, John Lufunga, Mtwawafu Kantangayo, Haleluya Ivody, Deocres Kagunila, Emmanuel Shitobelo, Happiness Rynyogote, Adolf Andrew, Adinani Musheruzi, Editha Domisian na Hashim Abdallah.
Biswaro alisema mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1) (b) na (2).
0 Comments