IDADI ya wanaume wakiwemo watumishi wa umma katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, ambao wameamua kuvunja ukimya, wakidai kupigwa na kutelekezwa na wenza wao, imeongozeka kwa kasi.
Mkuu wa Dawati la Polisi la Jinsia na Watoto Manispaa ya Sumbawanga, Koplo Germana Leo Mfwomi alieleza idadi hiyo imeongezeka kwa kasi baada ya gazeti hili kuripoti Agosti mwaka huu kuhusu ukatili wa kijinsia, wanaotendewa wanaume na wenza wao, ikiwemo kupigwa.
“Nimepata wateja wengi sana tangu gazeti hili lilipotoa taarifa ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa wanaume na wenza wao, ambapo sasa tayari wanaume 50 wameshafika kwenye dawati letu la polisi kutoa taarifa, awali walikuwa wakiona aibu sana ... kati ya hao wapo pia watumishi wa umma,” alieleza.
Koplo Mfwomi alilieleza gazeti hili kando ya kikao cha wadau, waliokuwa wakijadili ukatili wa kijinsia na kuaandaa Mpango Kazi kwa ajili ya kupinga ukatili huo. Kikao hicho kilifanyika jana katika Manispaa ya Sumbawanga na kuratibiwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Peace Relief Organization (PRO) kwa ufadhili wa Taasisi ya The Foundation for Civil Society, ambao unatekelezwa kwa awamu mbili.
Aliongeza kuwa wanaume hao hawana tena woga wala aibu, ambapo wamelieleza Dawati hilo la Polisi la Jinsia na Watoto jinsi wanavyopigwa huku wengine wengine wakieleza jinsi walivyopoteza viungo vyao ikiwemo meno baada ya kupigwa, hivyo kusababisha kuwa na mapengo kinywani.
Aliongeza kuwa wanaume wengine wameeleza kuwa wameamua kukimbia nyumba zao kutokana na kero wanazozipata kutoka kwa wenza wao, ambao hawako tayari kuachiwa fedha kidogo za matumizi wakati huu, ambapo hali ya maisha imekuwa ngumu (vyuma vimekaza), kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Ofisa Mradi wa PRO, Reuben Charles alisema kuwa mradi huo utatekelezwa katika kata zote 19 zilizopo Manispaa ya Sumbawanga. Katika awamu ya kwanza utatekelezwa katika kata 10 kwa kipindi cha miezi sita kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 60 .
|
0 Comments