Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa upanuzi wa mfumo wa ugawaji maji unaotekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Dawasa) wilaya hiyo kuongeza kasi katika ujenzi kukamilisha mradi kwa wakati.

Hapi ameiagiza Kampuni ya Majisafi na Majitaka (Dawasco) wilayani humo kutoa taarifa kwa wateja wao kuwa bili za makadirio wanazopelekewa bila huduma ya maji hawatalipa hadi watakapopata huduma hiyo.
Hapi alisema hayo jana alipotembelea maeneo mbalimbali unapofanyika ujenzi huo kujionea maendeleo ya mradi unaolenga kuongeza maji. Alisema ni muhimu wakandarasi kuongeza nguvu kukamilisha mradi huo na yupo tayari kutoa ulinzi ili wafanye kazi usiku na mchana.
Alisema mradi huo wa ujenzi wa Matanki ya kuhifadhia maji unakadiriwa kumaliza shida ya upatikanaji wa maji eneo hilo kwa asilimia 95. “Wananchi wengi bado wana shida kupata maji safi mategemeo yao sasa ni haya matanki.
Mradi huu ni wa fedha nyingi, Sh bilioni 80 za Serikali ya India za mkopo nafuu. Hakikisheni mnaenda na kasi ukamilike Februari. Wilaya yangu ipo tayari kuwapa ulinzi wa kutosha kama mtakuwa tayari kufanya kazi usiku na mchana,” alisema.
Hapi ameitaka Dawasa kusimamia kikamilifu mkataba wa mradi huo ili waweze kupata thamani halisi ya fedha iliyotolewa kwa mradi. Kuhusu Dawasco kutoa bili kwa wasiopata maji baada ya wananchi wa eneo la Changanyikeni kulalamikia kupewa bili bila maji kwa muda mrefu, Hapi aliagiza Dawasco kufuatilia malalamiko hayo na kuwaondoa kero wananchi.
Baada ya malalamiko hayo, Meneja wa Dawasco Mkoa wa Kawe, Judith Singinika alitoa ufafanuzi kwa wananchi hao akisema suala la kupelekwa kwa bili hizo linatokea katika maeneo yaliyounganishiwa huduma au miundombinu ya maji kama makadirio ya matumizi ambayo hulipi hadi upate huduma. “Kama umeletewa bili hizi za makadirio na huna maji hupaswi kulipa na ukihitaji ufafanuzi tembelea Dawasco kwa msaada,” alisema.