Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
MKUTANO wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliokuwa ufanyike Novemba mwaka jana, sasa umepangwa kufanyika Februari Kampala, Uganda.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa na uzito wa kipekee kutokana na viongozi wa EAC kujadili masuala ya miundombinu ndani ya nchi sita za EAC, afya na maendeleo yake kwa ujumla.

Mbali ya waasisi wa jumuiya hiyo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, wanachama wengine ni Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya EAC kwa umma, mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wajumbe zaidi ya 1,000 wa ndani na nje ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Wanatarajiwa kuzama katika kujadili masuala la miundombinu, fedha za tiba na maendeleo kwa kutumia kaulimbiu ‘Kukuza na Kupanua mtangamano kwenye miundombinu na maendeleo ya sekta ya afya nchi za EAC’.
Mkutano wa Kampala unaandaliwa na sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na nchi wanachama na wadau wakubwa wa maendeleo wa eneo hilo na wa kimataifa. Utakuwa wa kwanza wa wakuu wa nchi EAC, kuzungumzia masuala ya afya na wa nne kuhusu kugharamia miundombinu na maendeleo.
Mkuu wa Mawasiliano kwenye Sekretarieti ya EAC, Richard Owora Othieno kupitia taarifa yake alisema utajadili mambo ya manufaa kwa miundombinu na maendeleo ya afya, ikiwemo dhamira ya kugharamia, uwezeshaji kisiasa kutekeleza miradi, uwezekano wa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi na maendeleo ya mpango utekelezaji wa miradi.
Alisema wakuu wa nchi wanatarajiwa kuzungumzia maendeleo ya miradi miundombinu bora, ya uhakika, endelevu, imara na inayotolewa haraka ikiwemo wa kieneo na ile ya kuvuka mipaka, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi na hali bora za mwananchi.
Wakuu wa nchi pia wanatarajiwa kujadili uwezeshaji haraka wa usafiri bora EAC kupitia maendeleo ya mifumo inayoingiliana ya usafiri wa barabara, reli, mabomba, usafiri wa maji ndani ya nchi, viwanja vya ndege na bandari.
Kwenye sekta ya afya, wakuu wa nchi watajadili namna ya kuwa na uamuzi wa pamoja kuhusu vipaumbele vya uwekezaji kwenye sekta ya afya kwenye eneo hilo ili kutekeleza lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu, kutekeleza lengo la kumwezesha kila mtu kupata huduma za afya.