Marais John Magufuli na Paul Kagame wa Rwanda wakifurahia jambo.
USHIRIKIANO baina ya Tanzania na Rwanda umezidi kushika kasi, kuelekea kutanua wigo wa ukuaji sekta za biashara na ajira, baada ya juzi marais John Magufuli wa Tanzania na Paul Kagame wa Rwanda, kukubaliana kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ndani ya mwaka huu, iweze kuziunganisha nchi hizo haraka zaidi.

Ujenzi wa reli hiyo ya kisasa, mbali ya kuongeza kasi ya biashara baina ya nchi hizo mbili, kati ya sita zilizomo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), itazinufaisha pia nchi nyingine za EAC, Burundi, Uganda na jirani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo si mwanachama wa jumuiya ya EAC.
Nchi nyingine zilizomo katika jumuiya ya Afrika Mashariki ni Kenya na Sudan Kusini. Tayari Rwanda na Tanzania zinaunganishwa kwa uhakika kwa njia ya barabara ya lami na kwa anga kutoka Jijini Dar es Salaam.
Aprili mwaka jana, marais hao walizindua rasmi Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma ya Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo. Daraja hilo linakatisha Mto Kagera na kuunganisha nchi za Rwanda na Tanzania, hivyo kuongeza kasi ya usafiri na usafirishaji bidhaa na hivyo kukuza shughuli za kiuchumi.
Juzi Rais Magufuli alisema wamekubaliana kuanza ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) kati ya Isaka, Tanzania na Kigali, Rwanda yenye urefu wa kilometa 400 wakisisitiza ujenzi uanze ndani ya mwaka huu.
Aliwaambia waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam, kuwa tayari wamewaagiza mawaziri wa miundombinu, kukutana ndani ya wiki mbili kuanzia sasa ili kuweka mipango ya utekelezaji.
Alisema kumekuwa na ongezeko la mizigo ya Rwanda inayosafirishwa kupitia Tanzania inayokadiriwa kufikia tani 950,000 kwa mwaka. Hata hivyo, alisema biashara kati ya nchi hizi mbili siyo ya kuridhisha, hivyo wamekubaliana kuboresha zaidi mazingira ya biashara, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya reli na barabara.
“Tukijenga reli kutoka Isaka hadi Kigali, na sisi huku tunajenga kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na tukaunganisha Dodoma hadi Isaka, mizigo mingi ya Rwanda itasafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam, biashara itakua zaidi na ajira zitaongezeka,” Rais Magufuli alisema.
“Kule Rulenge Ngara, Burundi na Rwanda kote kuna madini ya nickel, tukijenga miundombinu yetu tutasafirisha madini haya na tutaongeza biashara. Na reli hii itatumiwa na nchi nyingine za Burundi, DRC na Uganda, kwa hiyo ni jambo muhimu sana kwa uchumi wetu na majirani,” alisema Rais Magufuli.
Tayari Tanzania imeshaanza ujenzi wa reli ya kisasa, huku awamu ya kwanza ya kilometa 205 ikianzia Dar es Salaam hadi Morogoro. Inajengwa na kampuni za Yapi Merkezi ya Uturuki na Mota-Engil ya Ureno kwa gharama ya Dola za Marekani bilioni 1.2 (Sh trilioni 2.7 za Tanzania) na kukamilika Oktoba 2019.
Itafuatiwa na sehemu nyingine nne, zitakazounganisha reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa urefu wa kilometa 1,219. Rais Magufuli anayechukuliwa kuwa ni mfano wa kuigwa kiuongozi ndani na nje ya Afrika, alimhakikishia Rais Kagame kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na Rwanda kwa manufaa ya wananchi na ipo tayari kumuunga mkono, atakapochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) katika kikao cha wakuu wa nchi na serikali mwishoni mwa mwezi huu huko Addis Ababa, Ethiopia viongozi watakapokutana.
“Rais Kagame nakupongeza sana, unafanya kazi kubwa ya kuwapigania wananchi wako, Watanzania tunajua ulikoitoa Rwanda na tunajua ulipoifikisha, nakuhakikishia tutaendelea kushirikiana katika jukumu la kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Rais Magufuli.
Rais Kagame alimshukuru mwenyeji wake, Rais Magufuli kwa mwaliko wake na kumpongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Tanzania.
Alisema yeye na Rais Magufuli, wameamua kufanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo na aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili mipango yote waliyojiwekea itekelezwe, ikiwemo kuinua biashara na kuongeza ajira, na alishukuru kwa kuwa tayari kumuunga mkono atakapochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AU.
UJENZI WAANZA
Aprili 12, mwaka jana, Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa sehemu ya kwanza ya reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa, itakayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, yenye urefu wa kilometa 300 zinazojumuisha vituo vya kupishana treni na vituo vya abiria na mizigo.
Pia ujenzi huo, utahusisha ujenzi wa uzio na vivuko vya watembea kwa miguu ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuwa treni itakayokuwa ikitumika ni ya umeme.
Reli inayojengwa itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa tani 35 kwa ekseli moja, itasafirisha abiria kwa mwendokasi wa hadi kilometa 160 kwa saa, mizigo kwa mwendokasi wa hadi kilometa 120 kwa saa na itakuwa na uwezo wa kusafirisha jumla ya tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka, ikilinganishwa na reli nyembamba iliyopo sasa iliyojengwa mwaka 1912 inayosafirisha abiria kwa mwendokasi wa kilometa chini ya 30 kwa saa, ikibeba tani 13 kwa ekseli moja na ina uwezo wa kubeba jumla ya tani milioni tano tu za mizigo kwa mwaka.
Itakuwa na uwezo wa kubeba treni inayovuta mabehewa 100 ya mizigo yenye urefu wa kilometa 2 kwa mpigo na mizigo itakayobebwa na treni moja ni sawa na mizigo, ambayo ingebebwa na malori 500 yanayopita barabarani.
Kupitia reli hiyo, abiria watasafiri kati ya Dar es Salaam na Morogoro kwa saa 2 na dakika 50. Kutokana na kuanza kwa mradi huo, Rais Magufuli alisema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia, kwani itasaidia kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo ndani ya nchi na kwenda nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na DRC ikizalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 600,000 na kuimarisha uchumi.
Rais Magufuli alisema kukamilika kwa reli hiyo, kutaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuwa na treni inayokwenda kasi (kilomita 160 kwa saa) na inayobeba uzito mkubwa zaidi ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ya pili barani Afrika kwa treni zinazokwenda kasi, baada ya ile ya Morocco ambayo inakimbia kwa kilomita 200 kwa saa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Kenya na Ethiopia walizindua treni zinazokwenda kasi ya kilomita 120 kwa saa, lakini treni ya Kenya inatumia mafuta na Ethiopia inatumia umeme.
Rais Magufuli alisema mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa ni wazi kuwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, treni hiyo itakuwa ikitumia chini ya saa 1:30 ambapo kwa basi kwa sasa ni zaidi ya saa 4:00.
Kwa mtu anayesafiri kwenda Dodoma sasa atalazimika kutumia saa 2:30 kufika makao makuu hayo ya nchi kutoka muda wa sasa wa saa nane hadi tisa kwa basi. Wakati kazi kati ya Dar es Salaam na Morogoro, ikiwa imeanza katika awamu ya kwanza, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema Serikali imetangaza zabuni ya ujenzi wa reli hiyo Morogoro hadi Makutupora (Dodoma) kilometa 336, Makutupora hadi Tabora kilometa 294, Tabora hadi Isaka kilometa 133 na Isaka hadi Mwanza kilometa 248.
Jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa alitangaza rasmi kuwa, uzinduzi wa ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya pili kuanzia Morogoro hadi Makutupora utafanyika mwezi ujao.
Aliliambia HabariLEO Afrika Mashariki kuwa, kuwa siku rasmi ya kuwekwa kwa jiwe la msingi itajulikana hivi karibuni taratibu zitakapokamilika. Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya kwanza, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu huyo wa Rahco alisema kuwa shughuli za ujenzi zinaendelea vizuri.
“Tunapoendelea na ujenzi katika hii awamu ya kwanza hatufanyi kitu kimoja, hivi karibuni tulitangaza hatua za manunuzi ya vichwa vya treni zinazotumia umeme, lakini pia shughuli za usanifu wa madaraja, usanifu wa njia yenyewe, usanifu wa umeme na usanifu wa makaravati unaendelea; lakini pia kwenye kambi yetu ya Ilala wameshaanza utengenezaji wa madaraja ya juu,” alisema Kadogosa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Hawa Ghasia alisema wakati wa uwekaji jiwe la msingi, usafiri wa reli ya kisasa na ya uhakika, utasaidia mambo mengi, hasa ujenzi wa uchumi imara utakaoipeleka nchi katika uchumi wa kati.
“Tuna bandari kubwa na maarufu Afrika Mashariki. Sasa ili tufaidike na hiyo bandari ni lazima tujenge reli na kuweka miundombinu mizuri ili kutoka kwenye ‘comparative advantage’ na kuwa ‘competitive advantage’ (faida za kiushindani) ili tupate faida ya kuwapo kwa bandari na tayari naona mwelekeo wa kufika huko,” alisema Ghasia katika hotuba.
UTAFITI EAC
Kwa mujibu wa utafiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ujenzi wa reli ya Isaka-Kigali utaigharimu Rwanda Dola za Marekani milioni 800 na 900 (kati ya Sh trilioni 1.7 na Sh trilioni 2 za Tanzania).
Aidha alisema utafiti unaonesha kuwa kwa reli ya aina hiyo, kama ingejengwa kuanzia bandari ya Mombasa, Kenya kupitia Uganda ingeweza kuigharimu Rwanda Dola za Marekani karibu bilioni 1 (Sh trilioni 2.2 za Tanzania).
Rwanda imesisitiza inakusudia kuzifanyia kazi njia zote, kupitia Tanzania na kupitia Rwanda ili kujihakikishia ufanisi katika usafirishaji wa bidhaa zake, lengo likiwa kwenda na wakati lakini pia kupunguza gharama za usafirishaji.
MIUNDOMBINU MINGINE
Mbali ya kuimarisha usafiri wa reli na kuufanya kuwa wa kisasa nchini, Serikali ya awamu ya tano pia imekuwa ikiendelea kujenga barabara kuu nchini kwa kiwango cha lami. Pia imeshanunua ndege kwa ajili ya Shirika la Tanzania Tanzania (ATCL) ili kuimarisha sekta ya usafiri wa anga.
Imejenga meli Ziwa Nyasa huku ikiwa katika mchakato wa kufanya hivyo katika Ziwa Victoria na pia Ziwa Tanganyika. Aidha, imeweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya usafiri katika majiji na miji nchini, mathalani, kwa Dar es Salaam, Serikali imechukua hatua madhubuti za kuboresha Jiji kwa kujenga barabara za juu katika makutano ya barabara maeneo ya TAZARA na Ubungo (Flyover), kujenga daraja la baharini litakalounganisha Aga Khan na ufukwe wa Coco Beach, kujenga barabara za mzunguko.
KANDA YA ZIWA
Kwa Kanda ya Ziwa, Serikali imepania kuifanya mikoa hiyo kuwa kitovu cha usafiri nchi za maziwa makuu kwa kuimarisha usafiri wa ndege, reli na meli katika Ziwa Victoria. Kanda hiyo inayoundwa na mikoa ya Mwanza, Mara na Shinyanga, inafikika kiurahisi na nchi jirani za Kenya, Rwanda, Burundi na DRC, hivyo pamoja na usafirishaji wa abiria na mizigo, Serikali iko mbioni kujenga uwanja wa kisasa, itajenga pia jengo jipya, kubwa na la kisasa la abiria katika kiwanja hicho ili abiria wa nchi za EAC wanaokwenda Ulaya, Mashariki ya Kati waanzie safari Mwanza.
“Uzoefu unaonesha abiria wengi wanaopanda ndege za Emirates katika nchi jirani wanatoka hapa kwetu,“ alisema Rais Magufuli mwaka jana akiwa mziarani mjini Mwanza ambapo alisisitiza hayo yanafanyika kama mchakato wa kuijenga Tanzania mpya, yenye uchumi imara.
Mfano, umbali kutoka Mwanza kwenda Kigali, Rwanda ni kilometa 549 kwa barabara kupitia mpaka wa Rusumo, mkoani Kagera na kwa ndege, ni umbali wa kilometa 322. Kutoka Mwanza kwenda Nairobi, Kenya ni kilometa 679 kwa barabara na kilometa 456 kwa ndege. Kwa usafiri wa barabara Mwanza kwenda Kampala, Rwanda kupitia Nairobi ni kilometa kwa 717, na ndege ni umbali wa kilometa 317